Unguja. Siku moja baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kueleza kuendelea kutumika utaratibu wa kawaida wa kura ya mapema, Chama cha ACT-Wazalendo kimewataka wananchi kisiwani humo watulie na suala hilo litashughulikiwa na viongozi wa chama hicho.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Agosti 19, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Ismail Jussa wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu Maalumu ya chama katika ofisi zake zilizopo Vuga kisiwani Unguja.
Jussa amesema, wananchi kisiwani hapo kwa sasa hawatakiwi kuchukua hatua yoyote juu ya uamuzi huo hadi chama kitakapotoa mwongozo.
“Suala la kura ya mapema tumeshalipigia kelele sana, hivyo tunachohitaji kwa Wazanzibari ni kuwa watulivu kwa sababu viongozi wao bado tunalifanyia kazi na ikifika wakati tutaelewana kwa kutoa mwongozo,” amesema Jussa.
Amesema, suala la kura ya mapema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 lilisababisha maafa makubwa, hivyo chama hicho hakiwezi kuliafiki hilo kwani hawataki yajirudie yaliyotokea awali.
Ameeleza kuwa, bado wananchi wa Zanzibar wanahitaji mabadiliko ya kweli na hawawezi kusimama mpaka lengo hilo litimie.
Jussa amesema, kati ya mambo matatu waliyohitaji kufanyiwa marekebisho miongoni mwao ni mfumo wa uchaguzi kufanya marekebisho ikiwemo kura ya mapema, fursa ya vitambulisho vya Uzanzibari kwa ambao wamenyimwa na marekebisho ya sektretarieti ya ZEC, huku akisema hayo yote hayajatekelezwa hadi kufikia sasa.
Hata hivyo, ametoa pongezi kwa wananchi kuwa wavumilivu na kuwa na misimamo thabiti ya kuhitaji mabadiliko na chama hicho ndio chenye dhima ya kuleta mabadiliko hayo.
Wakati jana akitangaza ratiba ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, Mwenyekiti wa ZEC, George Joseph Kazi amesema kura ya mapema itapigwa Oktoba 28.
Kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha sheria upigaji kura wa mapema utawahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi siku ya uchaguzi.
Hii siyo mara ya kwanza ACT Wazalendo kutoa kauli za kupinga hatua hiyo ya kura ya mapema katika chaguzi zilizopita.