Kesi anayedaiwa kujifanya ofisa polisi yakwama

Dar es Salaam. Kesi ya kujitambulisha kuwa ni askari polisi inayomkabili mfanyabiashara Msafiri Maulid (48), imeshindwa kuendelea na usikilizwaji, baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi.

Maulid, maarufu kama Msafiri Mahita na mkazi wa Mbezi Juu, anakabiliwa na shtaka moja la kujitambulisha kwa kepteni wa JWTZ kuwa yeye ni askari polisi na kuongozana na maofisa jeshi hilo kwenda nchini Uturuki kununua silaha, wakati akijua kuwa ni uongo.

Kesi hiyo ilipangwa leo, Agosti 19, 2025 kuendelea na usikilizwaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Frank Rimoy, ameieleza Mahakama hiyo kuwa hawana shahidi,  hivyo wanaomba wapangiwe tarehe nyingine ili waweze kupeleka mashahidi mahakamani hapo.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa mashahidi, lakini kwa bahati mbaya upande wa mashtaka hatuna shahidi kwa sababu tuliyemtegemea amepata udhuru, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi,” amesema Wakili Rimoy.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Aaron Lyamuya alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 1, 2025 itakapoendelea na usikilizwaji na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, Maulid anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 26, 2024 katika ofisi za Suma JKT, Jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa siku  ya tukio, mshtakiwa huku akijua kuwa yeye sio askari Polisi, alijitambulisha kwa kepteni Leslie Cheo kuwa yeye ni askari Polisi, wakati akijua ni uongo.

Baada ya kutambulisha kwa kepteni Cheo, mshtakiwa alijihakikishia na akuhusishwa katika mchakato wa ununuzi wa silaha na akasafiri hadi Uturuki akiwa na maofisa wa SUMA JKT ambapo walikamilisha ununuzi wa silaha.