Kibano wakwepa kodi kulipa mamilioni

Shinyanga.  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mtu yeyote atakayeingilia mfumo wa Mamlaka hiyo bila idhini adhabu yake kwa mtu binafsi ni kuanzia Sh20 milioni na kwa kampuni Sh60 milioni kutokana na kuisababishia hasara Serikali.

Hayo yameelezwa leo Agosti 19 na Ofisa Mkuu msimamizi wa kodi TRA, Hamad Mterry wakati akizungumza na wafanyabiashara ambao ni walipa kodi Manispaa ya Shinyanga wakati akieleza mabadiliko  ya sheria ya kodi ya mwaka 2025, ikiwemo sheria ya kuwabana watu wanaoingilia mfumo.

Amesema kumekuwa na tabia watu wanaingilia mifumo ya TRA na wakishaingilia wanafoji vitu wanaikosesha Serikali mapato, ambapo sasa kupitia sheria zilizowekwa zitawabana wanaofanya vitendo hiyo kwa kuchukuliwa hatua kali.

“Kwa kutumia mfumo wa kielekroniki utazalisha nyaraka za kieletroniki ambazo awali zilikuwa hazikubaliki Mahakamani, lakini kwa sasa kupitia mabadiliko ya sheria ya kodi ya mwaka 2025 zitakuwa ni nyaraka halali zitatambulika,” amesema.

Amesema badiliko lingine ni mifumo kusomana ambapo mfanyabiashara anapokuwa na mifumo yake na TRA ni lazima mifumo hiyo isomane hiyo ni sheria na siyo kuomba kama ilivyokuwa zamani kama ambavyo wafanyabiashara wanasoma ya mamlaka hiyo wakiwa nyumbani ndivyo hivyo na wao wasome wakiwa ofisini.

Mterry amesema kupitia mabadiliko hayo ya sheria kitambulisho cha mjasiriamali kimefutwa ambapo kila mfanyabiashara atatakiwa kuwa na tini namba ambazo zitaonesha kuwa ni mfanyabiashara mdogo huku mamalishe na bodaboda wameondolewa kodi.

Mwenyekiti wa jukwaa la wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga, Jacton Koyi ametoa ushauri kwa TRA kuendelea kuwa karibu na walipa kodi kuwapatia elimu ambapo pia amewaomba wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya nchi.

Zenaida Rweisunga mfanyabiashara wa chakula mamalishe amepongeza hatua hiyo ambayo itawasaidia  wafanyabiashara kupiga hatua na kuwawezesha kufanya shughuli za maendeleo ambazo zitachangia kukuza uchumi wa nchi.