Dar es Salaam. Chama cha Watanzania waliohitimu katika Chuo Kikuu cha Bahari Duniani (WMU) kinakusudia kuwaleta pamoja wataalamu katika sekta hiyo ili kushirikiana kitaaluma na kusaidiana katika kushughulikia changamoto na fursa katika sekta ya bahari kitaifa na kikanda.
Chama hicho kinachojulikana kama Chama cha Wahitimu wa WMU Tanzania (WMUTAA), kilisajiliwa rasmi Aprili 2025 baada ya kutimiza matakwa yote ya kisheria chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kupitia umoja wao, wataalamu hao wanakusudia kuimarisha ushirikiano, ubadilishanaji wa maarifa na matumizi ya utaalamu walioupata katika ngazi ya kimataifa.
Akizungumzia malengo yao, Agosti 19, 2025, mwenyekiti wa mpito wa chama hicho, Profesa Tumaini Gurumo ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI), amesema ni kutoa ushirikiano kwenye sekta ya bahari hapa nchini.
“Lengo letu ni kuunganisha wahitimu wote wa WMU, kushirikiana kitaaluma na kutumia utaalamu tulio nao kushughulikia changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya bahari. Tunataka kuhakikisha kwamba maarifa na uzoefu wetu vinatumika kuendeleza sekta hii kwa faida ya taifa na kikanda,” amesema Profesa Tumaini.
Amesema chama hicho kitakuwa jukwaa la kushirikiana, kubadilishana uzoefu na maarifa na kusaidia wahitimu wote wa WMU Tanzania kuleta mchango chanya katika maendeleo ya sekta ya bahari, si tu hapa nchini bali pia kimataifa.
Kwa upande wake, mmoja wa wahitimu kutoka katika chuo hicho, Grace Mroso amesema: “Kama mhitimu wa WMU, nimejifunza mengi kuhusu usimamizi wa meli, sera za bahari na ubora wa mazingira ya bahari. Kuanzishwa kwa WMUTAA ni fursa kubwa kwetu kushirikiana na kuendeleza sekta ya bahari nchini Tanzania.
Mtaalamu huyo wa bahari ameongeza kuwa: “Tunataka kutumia utaalamu tulionao kuleta mabadiliko chanya na kusaidia kutatua changamoto za kitaaluma na kiutendaji.”
Ameongeza kuwa wanajivunia kuwa sehemu ya jukwaa la kimataifa linalounganisha wahitimu wa WMU na kwamba hiyo itawaruhusu kutambua fursa mpya za ushirikiano, kubadilishana maarifa na kuimarisha sekta ya bahari kupitia uzoefu wao wa kimataifa.
Chama hicho kinatarajiwa kukizinduliwa rasmi Agosti 21, 2025 jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Chuo Kikuu Bahari Duniani, Profesa Maximo Mejia.
WMUTAA kinaundwa na Watanzania 160 waliohitimu WMU, wakiwa wamebobea katika nyanja mbalimbali kama elimu na mafunzo ya bahari, usimamizi wa meli na bandari, sheria na sera za bahari, usimamizi wa nishati za bahari na mazingira ya bahari.
Chama hicho kinaongozwa kwa sasa na uongozi wa mpito uliochaguliwa kwa makubaliano ya pamoja ambapo Profesa Tumaini kutoka DMI ni Mwenyekiti na Dk Gerson Fumbuka ni Katibu Mkuu.