Mafuriko yaua watu watatu, yaacha zaidi ya 100 bila makazi

Kampala. Watu watatu wamefariki dunia huku zaidi ya watu 100 wakipoteza makazi baada ya mafuriko makubwa kuyakumba maeneo ya Mbale na Sironko nchini Uganda.

Taarifa iliyotolewa na tovuti ya habari ya Daily Monitor ya Uganda imeeleza kuwa mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha tangu Jumapili, Agosti 17, 2025, na kusababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara na madaraja.

Pia, mafuriko hayo yameharibu mazao katika baadhi ya mashamba na kuacha takriban watu 100 bila makazi, baada ya nyumba zao kuzama maji na nyingine kuharibiwa kabisa.

Tovuti hiyo pia inaeleza kuwa daraja la Nalugugu lilivunjika kutokana na nguvu ya maji, jambo ambalo limesababisha changamoto kubwa katika usafiri wa barabara ya Kapchorwa kwenda Mbale.

“Daraja hilo ambalo ni kiunganishi muhimu kati ya eneo la Bugisu, Sebei na Karamoja, hivyo baadhi ya madereva walikwama eneo hilo.

“Malori makubwa, mabasi na magari ya mizigo yalilazimika kuegesha pande zote mbili za barabara, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari,” imeeleza tovuti hiyo.

Naibu Mkuu wa Wilaya ya Sironko, Allan Wortalwa, amesema polisi wa usalama barabarani wamepelekwa eneo hilo na wameanza kuruhusu pikipiki na magari madogo pekee  kupita.

“Muundo wa daraja umedhoofika na si salama kwa magari makubwa, tunashirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha wanaopita katika maeneo hayo wanakuwa salama,” amenukuliwa na tovuti hiyo.

Naibu kamishna wa jiji, Alfred Chebet amesema mito ya kwenye eneo hilo ilivunja kingo na kusomba miundombinu hivyo  kusababisha barabara kufungwa.

“Kamati yetu ya usimamizi wa maafa inafanya tathmini ya kiwango cha uharibifu wa miundombinu na makazi uliotokea,” amenukuliwa na tovuti hiyo.

Wakati huohuo, Idara ya Hali ya Hewa ya Wizara ya Maji na Mazingira imetoa onyo la kuendelea kwa mvua kubwa mashariki mwa nchi hiyo, huku ikiwataka wakazi wa maeneo yanayokumbwa na mafuriko kuchukua tahadhari.