Vyombo vya habari nchini Finland vimeripoti kuwa Mbunge wa Chama cha Kidemokrasia cha Kisoshalisti (SDP), Eemeli Peltonen(30) amejinyonga ndani ya jengo la Bunge nchini humo.
Gazeti la Iltalehti, ambalo ndilo la kwanza kutoa taarifa hizo, limesema mtu mmoja alifariki dunia saa 5 asubuhi leo Jumanne Agosti 19, 2025 ndani ya jengo la Bunge, jijini Helsinki.
Ingawa mamlaka zimetangaza tu kifo cha mtu mmoja bila kutoa maelezo zaidi, vyombo vya habari vya ndani vimethibitisha mtu huyo kuwa ni Mbunge wa Chama cha Kidemokrasia cha Kisoshalisti (SDP), Eemeli Peltonen na kwamba alijiua.
Polisi wanaochunguza tukio hilo wamesema hawana mashaka ya kuwepo kwa mchezo mchafu, huku wahudumu wa afya wakiwahi kufika eneo la tukio baada ya kupokea simu saa 5:06 asubuhi. Mashuhuda wamesema waliona magari ya wagonjwa yakielekea nyuma ya jengo la Bunge yakiwa na ving’ora, yakifuatiwa na gari kubwa la zimamoto, gari la polisi na baadaye gari la polisi la kivita aina ya Mercedes.

Mkurugenzi wa Usalama wa Bunge, Aaro Toivonen, hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo, akisema tu kuwa: “Kuna operesheni inaendelea kwa kushirikisha vikosi vya uokoaji, polisi na huduma za dharura. Siwezi kusema zaidi kwa sasa. Bunge ni eneo la kipekee, hivyo hatua mbalimbali za dharura huchukuliwa kila inapokuwa na hali isiyoeleweka.”
Waziri Mkuu wa Finland, Petteri Orpo, akizungumza kuhusu msiba huo, amesema chama chake tawala cha Coalition Party kitaacha kujadili siasa kwa muda kama ishara ya maombolezo.
“Tumepokea taarifa za kushtua sana kutoka bungeni, mahali petu pa kazi, kwamba mmoja wa wenzetu amefariki dunia humohumo. Habari hizi ni za kuhuzunisha sana,” amesema.
Bunge la Finland kwa sasa lipo mapumzikoni na linatarajiwa kuanza vikao vyake Septemba 2, mwaka huu.