KAMPUNI ya Mookh Africa imewaomba radhi mashabiki wa soka nchini Kenya baada ya mfumo wake wa mtandaoni kushindwa kufanya kazi ipasavyo wakati tiketi za michuano ya CHAN zilipoanza kuuzwa jana, saa 6 mchana.
Tiketi hizo ni kwa ajili ya mechi ya robo fainali kati ya Harambee Stars ambayo iliongoza kundi A dhidi ya Madagascar ambayo ilishika nafasi ya pili nyuma ya Tanzania kundi B. Mechi hiyo itachezwa Ijumaa ya Agosti 22, Kasarani, Nairobi.
Kupitia taarifa yao kwa umma, Mookh Africa imesema mfumo wao ulivamiwa na ‘bots’ (programu za kiotomatiki) ambazo ziliwazuia mashabiki halisi kupata tiketi, hali iliyosababisha malalamiko kwenye mitandao ya kijamii.
“Tumejua jinsi ilivyo muhimu kwa mashabiki kupata nafasi ya haki ya kununua tiketi. Tumelisikia tatizo,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mookh ilieleza kuwa mara tu uuzaji wa tiketi ulipofunguliwa, mashine za kiotomatiki ziliushambulia mfumo, jambo lililosababisha mashabiki wengi kushindwa kupata tiketi walizozisubiri.
“Timu yetu inaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa tiketi zinafika kwa mashabiki wa kweli, siyo kwa ‘bots’,” waliongeza.
Kampuni hiyo imewapongeza mashabiki kwa uvumilivu wao huku ikiahidi kurejesha huduma hiyo mtandaoni haraka iwezekanavyo.