MWEZI mmoja kabla ya Mlandege kuifuata Insurance ya Ethiopia, wawakilishi hao wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika wanahaha kuwatafutia wachezaji wa kikosi hicho utambulisho wa uraia na hati ya kusafiria pasipoti kutoka wengi wao kutokuwa na vitambulisho vya Nida.
Mabingwa hao wa Ligi ya Zanzibar inatarajia kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Septemba 19-26 ikianzia ugenini.
Mapema leo Mwanaspoti limehudhuria mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea visiwani Unguja na kushuhudia viongozi wakihaha kuzungumza na wachezaji kwa ajili ya kukamilisha mpango huo ambao inaelezwa kuwa hapa Zanzibar imeshindikana suala la hati ya kusafiria na wana mpango wa kuvuka maji hadi Bara.
Katika hali isiyo ya kawaida kuna baadhi ya wachezaji ndani ya timu hiyo hawana hati ya utambulisho wa uraia kitambulisho cha Nida, hivyo wanafanya mchakato wa kwenda mahakamani kuapa ili kutengenezewa hati ya kusafiria.
Inaelezwa mchakato huo wa kupambania hati za kusafiria pamoja na kitambulisho cha Nida kwa wachezaji wao umeanza tangu jana Jumatatu na wanaendelea kupambana ili waweze kufikia malengo.
Mmoja wa kiongozi wa timu hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia Mwanaspoti, kuna wachezaji saba wataenda Bara kwa ajili ya kushughulikia hati za kusafiria.
“Mambo magumu tunapambana wachezaji wote wanatakiwa kuwa na hati za kusafiria na Nida, hadi muda huu bado hatujafanikiwa kuwasajili wachezaji watakaoiwakilisha Zanzibar kimataifa katika mfumo mambo ni mengi ila tunapambana.”