NAMUNGO FC inaendelea kujifua katika kambi iliyopiga jijini Dodoma kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, huku ikiwa na matarajio ya kucheza mechi mbalimbali za kirafiki.
Katibu wa Namungo, Ally Seleman alisema timu ilianza mazoezi Jumatatu wiki hii chini ya kocha msaidizi Ngawina Ngawina, kisha baada ya siku tatu wataanza kucheza mechi za kirafiki.
“Tulifika Dodoma Jumapili, Jumatatu timu ilifanya mazoezi, baada ya hapo tutaanza kutafuta timu za kucheza nazo mechi za kirafiki, tutayafanya hayo kwa mahitaji ya kocha kwa kile ambacho atatuelekeza,” alisema na katibu huyo na kuongeza.
“Maandalizi ya msimu yamebeba vitu vingi, hapo ndipo timu inapotengenezwa kiushindani, ukizingatia Ligi Kuu imekuwa ngumu, tunaamini msimu ujao hautakuwa mwepesi, lazima kocha akiandae kikosi ipasavyo ambacho kitakuwa kinatupa matokeo ya ushindi.”
Nyota wa timu hiyo, Pius Buswita kuhusu maandalizi hayo alisema: “Tutapata muda mzuri wa kutuliza akili zetu na kujiandaa kwa mapambano ya msimu ujao. Binafsi nilimaliza ligi na mabao matatu, hivyo natamani kufunga mengi zaidi ili niwe kati ya wachezaji watakaokaa katika rekodi ya wenye mabao mengi.”
Kwa upande wa beki Hussein Kazi aliyejiunga na timu hiyo akitokea Simba, alisema: “Bado ni mapema lakini natarajia tutakuwa na kambi nzuri na msimu ujao utakuwa wa mapambano zaidi.”