Prisons, Mbeya City zakimbia Jiji, tambo zatawala

WAKATI presha ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ikipamba moto, Mbeya City na Tanzania Prisons zimetimka jijini Mbeya kwa ajili ya maandalizi yao, huku matumaini ya kufanya vizuri kwa pande zote yakiwa makubwa.

Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/26 inatarajiwa kuanza Septemba 16 mwaka huu na mkoani Mbeya timu mbili zinatarajiwa kuwakilisha kwenye michuano hiyo ambazo ni Prisons na Mbeya City iliyorejea baada ya kukosekana misimu miwili kutokana na kushuka daraja.

Katika historia, Mbeya iliwahi kuwa na timu nne Ligi Kuu msimu wa 2021/22 ambazo ni Prisons, Mbeya City, Ihefu (iliyouzwa na sasa Singida Black Stars) na Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja baada ya kushiriki msimu mmoja tu kwenye michuano hiyo.

Hadi sasa, Prisons na Mbeya City zimeshaondoka Mbeya Mjini na kujificha maeneo tofauti na ‘Wajelajela’ wameweka kambi yao Kiwira, huku ndugu zao City wanaomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wakijifua Mwakareli.

Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota alisema kambi hiyo itadumu kwa wiki nne ambapo mazingira waliyoweka wanaamini itawapa mafanikio kwani hakuna muingiliano na benchi la ufundi linafanya majukumu yake.

Alisema baada ya kambi hiyo, timu itarejea kwa mechi za kirafiki pamoja na kushiriki matukio muhimu, akiwaomba mashabiki kuendelea kuisapoti Mbeya City ili kupata furaha.

“Tumeamua kujificha huko ili kuwapa wachezaji na benchi la ufundi kufanya majukumu yao bila kuingiliwa, baada ya wiki nne hivi, tutarejea mjini kwa ajili ya matukio yaliyoandaliwa ikiambatana na michezo ya kirafiki, matarajio yetu ni kufanya vizuri,” alisema Mwankota.

Ofisa Habari wa Prisons, Alexander Ngelela alisema timu hiyo inatarajia kuwa Kiwira kwa siku saba kisha kuamuliwa uelekeo wa sehemu nyingine kwa ajili ya maandalizi ya ligi.

“Tunaweza kwenda Dar es Salaam au Babati mkoani Manyara na tutashiriki michuano iliyoandaliwa kwa baadhi ya timu takribani tisa, lakini yote itategemeana na mipango na uamuzi wa uongozi na benchi la ufundi.

“Tumeamua kwenda Kiwira kwani ni maeneo yenye usalama na tumezoea kila msimu kuanza tunaweka kambi huko, matarajio ni kuona tunafanya vizuri kwa sababu tumesajili vyema kulingana na mahitaji yetu,” alisema Ngelela.