SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) limepanga kuweka sheria mpya itakayowalazimisha waandaaji wa mashindano ya mchezo huo kuhakikisha wanajumuisha pia mbio za watoto katika kila tukio litakaloandaliwa.
Hatua hiyo inalenga kujenga msingi imara wa vipaji na kuwekeza mapema kwenye maendeleo ya riadha nchini.
Rais mpya wa RT, Rogath John Stephen Akhwari alisema mpango huo utahusisha kuandaa mashindano maalumu ya watoto na vijana kwa kila kanda, yakiratibiwa kwa kushirikiana na vyama vya mikoa ili kuhakikisha kunakuwepo mtiririko wa mashindano kuanzia ngazi ya chini.
Akhwari alibainisha wapo mbioni kuandaa kanuni mpya za kusimamia mbio za barabarani nqa kutakuwa na utaratibu wa kutofautisha mashindano ya kimaifa yatakayosimamiwa na RT moja kwa moja na yale ya ndani yenye malengo ya kitaifa, kwa lengo la kuongeza ubora na hadhi ya riadha nchini.
“Hizi mbio itakuwa ni lazima, siyo chaguo, tunataka kuboresha kanuni zetu na yeyote atakayehitaji kibali cha kuandaa mashindano atalazimika kuhakikisha mbio za watoto pia zitakuwepo,” alisema Akhwari.
Alieleza watapeleka wataalamu waliobobea ili kusaidia wandaaji kuelewa namna sahii ya kuandaa mashindano ya watoto, akisisitiza changamoto kubwa iliyokuwepo awali ni watoto kukimbia mbio ndefu zisizolingana na umri wao.
“Watoto wetu wamekuwa wakikosa fursa hizi kwa sababu mara nyingi wakipewa mbio wanakimbizwa umbali wa kilometa tano, hapo awali tulivumilia kwa sababu tulikuwa hatuna mfumo madhubuti, lakini sasa tunataka kubadilisha hilo,” aliongeza.
Aidha kabla ya sheria mpya kupitishwa, RT imesema itatoa elimu kwa waandaaji wote wa mbio na kuwapa muda wa maandalizi kabla ya utekelezaji rasmi.
Akhwari anasema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha riadha Tanzania inakua kwa kuanzia watoto, vijana hadi kuzalisha wanariadha wa kiwango cha kimataifa.