MSHAMBULIAJI Wazir Junior Shentembo ameweka wazi sababu ya kurejea Dodoma Jiji, anataka kumaliza mkataba wake wa mwaka mmoja kisha atimke nje.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga na KMC, msimu uliopita kabla ya kutimkia Al Minaa ya Iraq alipocheza kwa mkopo wa miezi sita, alikuwa akiitumikia Dodoma Jiji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Waziri Jr alisema kwenye kikosi hicho kulikuwa na nafasi ya kusajiliwa lakini kama mchezaji huru na hilo ndilo limemkwamisha akaamua kurejea nchini kumaliza mkataba wake na Dodoma Jiji.
“Nimeamua kurudi Dodoma ili nimalizie mkataba wangu wa mwaka uliobaki, ukiwa mchezaji huru hakuna pingamizi nyingi wala vikwazo kama timu imekutaka na kuamini uwezo wako,” alisema na kuongeza.
“Nimepata timu kama tatu hivi ikiwemo Saudi Arabia, hivyo nikimalizana na Dodoma, mipango inayofuata ni kuangalia ofa gani nzuri baada ya hapo nitasepa.”
Waziri alisema kwa miezi sita aliyokaa Iraq amejifunza vitu vingi hasa ukomavu uwanjani licha ya kutopata nafasi ya kucheza.