Kibaha. Shule ya Msingi Miembesaba iliyopo Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi, hivyo imewaangukia wadau ikiomba msaada wa kujengewa vyoo vya kisasa.
Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 944 na walimu 24, inahitaji matundu 39 ya vyoo, kwa sasa yapo saba pekee, jambo linasababisha msongamano wa wanafunzi vyooni na kuhatarisha afya zao.
Ombi hilo limetolewa leo Agosti 19, 2025 na Mkuu wa Shule hiyo, Jairos Doha wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati wa hafla ya kupokea msaada wa meza na viti kutoka benki ya NMB kwa ajili ya walimu na wanafunzi.
Amesema licha ya msaada huo, shule inakabiliwa na uhaba wa matundu ya vyoo ambapo kwa sasa yaliyopo ni saba kati ya 39 yanayohitajika, hali inayowapa wakati mgumu wanafunzi wanapohitaji huduma hiyo.
“Tunashukuru kwa msaada huu, lakini tunalia na changamoto ya vyoo. Tukisaidiwa pia upande huo, itakuwa faraja kubwa,” amesema Doha.
Kwa upande wake, Ofisa Taaluma wa Manispaa ya Kibaha, Adinan Luvamba ameunga mkono ombi hilo akisema changamoto hiyo inapaswa kuangaliwa kwa jicho la pili ili kuwasaidia wanafunzi hao.
Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio amesema benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida kusaidia jamii katika elimu, afya na majanga mengine.
Amesema benki hiyo kama ilivyo desturi yake ya kusaidia jamii, itaendelea kufanya hivyo ikiwa ni mpango wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupunguza changamoto za jamii.
“Sisi tunaendelea kusaidia jamii na hiyo ni jadi yetu ili kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kupunguza changamoto kwa jamii,” amesema.
Mgeni rasmi aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Remita Luzabika ameipongeza NMB na kuwataka walimu kutunza msaada huo kwa manufaa endelevu.

Benki hiyo imekabidhi jumla ya viti na meza 60 ambavyo vimegharimu Sh19 milioni vitakavyogawanywa kwa shule nne ambazo ni Miembesaba, Mkoleni, Mbwawa na Miswe.