Dar es Salaam. Baada ya kusakamwa kutovaa suti kwenye mkutano wa Rais Donald Trump uliopita, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy hatimaye katika mkutano wa jana wa kutafuta amani ya Ukraine na Russia, alionekana amevaa suti ya kijeshi hatua iliyoibua mada mpya.
Katika mkutano uliopita mapema mwaka huu kati ya Trump na Zelenskyy na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance katika Ofisi ya Oval, ulipofika wakati wa maswali ya waandishi, mmoja alimuuliza kwa nini hakuvaa suti na je, anamiliki suti? swali lililozua mjadala hasa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Nitavaa vazi hilo baada ya vita hivi kumalizika,” Zelenskyy alijibu akimaanisha vita ya Ukraine na Russia iliyoanza tangu Februari 2022.

Hata hivyo, katika mkutano wa jana Jumatatu Agosti 18,2025 kati yake Zelenskyy, Trump na viongozi wa Ulaya alionekana akiwa ndani ya suti yenye koti la kijeshi la mifuko minne ikiwa ni muundo uliobuniwa na mbunifu wa Ukraine, Viktor Anisimov. Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian.
Ingawa baadhi ya waandishi walidhani ni suti ya kawaida, Anisimov alieleza kuwa ni jaketi la kijeshi lililotengenezwa kwa kitambaa cha canvas.
Zelenskyy, ambaye mara nyingi amekuwa akivalia mavazi ya kijeshi tangu Russia ilipoivamia nchi yake mwaka 2022, alisema mapema mwaka huu hatavaa suti ya kiraia hadi vita vitakapomalizika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Anisimov, uamuzi wa kubadili mtindo ulianza kuandaliwa Januari, kabla ya mkutano wake mgumu wa kwanza na Trump Februari, ambapo alikosolewa kwa kuvaa shati la mikono mirefu la kijeshi.

Mbunifu huyo alisema lengo ni kubadilisha taswira ya Zelenskyy taratibu kuelekea mtindo wa kiraia huku akibaki na taswira ya kijeshi kama ishara ya mshikamano na wananchi wake.
Wakati wa mkutano wa Jumatatu, mwandishi wa televisheni, Brian Glenn, ambaye awali alimkosoa Zelenskyy, safari hii alimsifia: “Unaonekana mzuri”. Trump naye akaongeza kwa kusema: “Nimesema hivyohivyo.”
Kwa upande wake, Zelenskyy alimjibu Glenn kwa utani: “Mimi nimebadilika, wewe hujabadilika.”
Licha ya mijadala kuhusu mavazi, Anisimov alisisitiza kwamba kilicho muhimu zaidi si suti wala mtindo, bali matokeo ya mazungumzo kuhusu mustakabali wa Ukraine.