Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa mwongozo na maelekezo kuhusiana na usambazaji wa maudhui na jumbe za mkupuo kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mwongozo huu umekuja ikiwa zimesalia siku 10 kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, ubunge na udiwani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Kampeni za uchaguzi mkuu unaosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amesema mwongozo huo unalenga kuhakikisha maudhui yanayotolewa kwa wananchi yanadumisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.
Miongoni mwa mambo yaliyoelekezwa kwenye mwongozo huo ni watoa huduma za mawasiliano ya simu na wanaoandaa jumbe hizo kuhakikisha maudhui yake, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 yanazingatia sheria na kanuni zote za mawasiliano ya kielektroniki na posta.
Lingine ni uhakiki wa maudhui kabla ya kusambaza jumbe za mkupuo zinazohusika ili kuhakikisha hakuna ujumbe wenye kuchochea vurugu, uvunjifu wa amani au kueneza taarifa za uongo unaowafikia watumiaji wa huduma za mawasiliano.
Mamlaka hiyo pia imeelekeza maudhui yote yanayohusiana na shughuli za uchaguzi mkuu yapate idhini kutoka kwa taasisi au uongozi wa chama cha siasa husika.
Msisitizo umetolewa pia kwa watoa huduma kuhifadhi kumbukumbu za ujumbe wote unazotumwa kwa wingi kwa kipindi kinachotakiwa kisheria kwa ajili ya uthibitisho endapo utahitajika.
Dk Bakari ameonya vikali watoa huduma za maudhui mtandaoni wanaosambaza habari na matukio bila ya leseni ya mamlaka akieleza watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria.
Mkurugenzi huyo amesema wanaofanya hivyo wanakiuka Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2022.
“TCRA ina wajibu wa kusimamia huduma za mawasiliano ya simu na intaneti, Posta, na utangazaji wa redio, televisheni na maudhui mtandaoni. Tumekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa utoaji huduma za maudhui mtandaoni kama sehemu ya mamlaka iliyopewa na EPOCA na Kanuni zake,” amesema Dk Bakari.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Josephat Mutabuzi amesema hatua hiyo inaleta uwajibikaji na uadilifu katika mchakato wa mawasiliano ya kisiasa, huku akitahadharisha usiwe kikwazo kwa vyama vidogo kufikisha ujumbe wao kwa wananchi.
“Mara nyingi tumeshuhudia taarifa za kupotosha zikisambazwa wakati wa uchaguzi. Mwongozo huu utasaidia kupunguza taharuki na hofu kwa wananchi. TCRA ihakikishe taratibu hizi haziwazuii wanasiasa wadogo kutumia njia za kidijitali kujitangaza,” amesema Mutabuzi.
Kwa upande wake, Zainab Juma ambaye ni mchambuzi wa masuala ya mawasiliano ya kidijitali, amesisitiza umuhimu wa TCRA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kuelewa mipaka ya matumizi ya mawasiliano wakati wa uchaguzi, wakisema elimu ya uraia ni nguzo muhimu ya kudumisha amani.
“Changamoto kubwa ni ukaguzi na ufuatiliaji na elimu, watu wafundishwe matumizi sahihi ya mawasiliano baada ya hapo TCRA ishikilie msimamo wake kuhakikisha watoa huduma hawapitishi ujumbe bila uhakiki, vinginevyo itakuwa kazi bure,” amesema.