Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Simanjiro.

Na Mwandishi Wetu, Simanjiro.
● Ujenzi wa soko la madini Mirerani umefikia 98%.
● Shilingi bilioni 5.5 zimetolewa na Rais Samia kukamilisha mradi
● Shughuli za biashara kuanza rasmi Septemba 15, 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amemtaka mkandarasi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha unakamilisha mapema ujenzi wa jengo la soko la madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, kufikia mwishoni mwa Agosti mwaka huu.
RC Sendiga alitoa agizo hilo jana Agosti 18, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi huo, ambapo hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.
Jengo la Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara, likiwa katika hatua za mwisho za ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akikagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Wilaya ya Simanjiro
Jiwe la Msingi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bi. Mariam Muhaji, akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Wilaya ya Simanjiro.
—
“Hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huu, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan tayari ametoa zaidi ya shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kukamilisha soko hili,” alisema Sendiga.
Aidha, alielekeza kuwa kufikia Septemba 15, 2025 shughuli rasmi za uuzaji na uchakataji wa madini zianze katika soko hilo, akisisitiza kuwa litakuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Mirerani na Wilaya ya Simanjiro kwa ujumla.
Katika kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa bora, RC Sendiga alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Simanjiro kusimamia maboresho ya ndani na nje ya eneo la soko, huku akisisitiza viwanja vya biashara vinavyozunguka eneo hilo vitolewe bila urasimu.
“Viwanja hivi ni mali yetu wananchi wa Mirerani. Tuelezwe wazi masharti ni yapi ili wananchi wajipange mapema. Tunataka faida ya kwanza ibaki kwa wananchi wa hapa,” alisisitiza.
Vile vile, RC Sendiga aliwataka viongozi na wananchi kuendelea kulitangaza soko hilo ili liwe kitovu cha biashara na uwekezaji wa madini aina ya Tanzanite.
Katika hatua nyingine, aliwakumbusha wakazi wa Mirerani na Simanjiro kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.