Vipaumbele vinne Dk Biteko akizindua mpango kazi ajenda ya wanawake

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amezindua mpango kazi wa kitaifa wa kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama  2025-2029 huku akianisha vipaumbele vinne vilivyo kwenye mpango huo.

Vipaumbele hivyo ni  kuwafundisha namna ya kuzuia changamoto wanazokutana nazo, kushirikishwa namna ya kuzikabili, kuwalinda ili waendelee wawe salama na kuwa msaada wa urejeshaji wa hali ya ustawi kwa mwanamke.

Akizungumza leo Jumanne Agosti 19, 2025 katika hafla ya uzinduzi huo uliohudhuliwa pia na viongozi mbalimbali, akiwamo mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Woman), mabalozi wa baadhi ya nchi na taasisi mbalimbali, Dk Biteko amesema mpango kazi huo ni nyenzo ya kupiga hatua katika ajenda ya wanawake, amani na usalama.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania kilichopo Kunduchi jijini hapa, Dk Biteko amesema mpango kazi huo umeandaliwa na wataalamu wabobezi.

Akiuchambua amesema: “Una sehemu sita, sehemu ya pili ndiyo inatoa uchambuzi wa kina wa hali halisi ya masuala ya wanawake kwenye nchi yetu kwa kupitia tafiti za kina.”

Naibu waziri mkuu huyo amesema tafiti zinaonesha asilimia 48.3 ya wanawake nchini wamewahi kufanyiwa ukatili wa aina fulani kwenye maisha yao.

Dk Biteko amegusia pia ukatili ambao wanawake waliokwenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa 2015.

“Tafiti zinaonesha asilimia 65 walikutana na changamoto mbalimbali zikiwamo za matusi. Asilimia 17 ya wanawake waliokwenda kugombea nafasi mbalimbali walishambuliwa kimwili wakati asilimia 13 waliombwa rushwa ya ngono,” amesema.

Amesema mambo hayo lazima yawekewe mkakati wa kuyazuia, “ndio maana katika vipaumbele vinne kwenye mpango huu, cha kwanza ni kuzuia, haipaswi mwanamke kuwa mtu wa kunyanyaswa katika jamii ambayo imetokana na huyo huyo mwanamke.” Amesema sura ya pili kwenye mpango huo inaonesha kila mmoja ana wajibu wa kuinua hadhi ya wanawake na watoto.

Hata hivyo, amegusia namna Serikali inavyochukua hatua za mara kwa mara ikilenga kunyanyua hadhi ya mwanamke.

“Mtakumbuka Tanzania imeendelea kuwapa wanawake fursa za juu na za uamuzi katika eneo hili la ajenda ya wanawake, amani na usalama. Katika mkakati huu, tumejulishwa kuwa, hadi kufikia Mei, 2023 uwakilishi wa wanawake katika mfumo wa Mahakama umefikia asilimia 46.6 vilevile hadi kufikia Juni 2023, wanawake ni asilimia 24.5 ya mabalozi na ofisi nane za kibalozi kati ya 33, zinaongozwa na wanawake,” amesema Dk Biteko.

Akizungumzia nafasi ya mwanamke ndani ya Jeshi la Polisi, Dk Biteko amesema asilimia 22 ya askari polisi ni wanawake na asilimia 30 ya maofisa uhamiaji ni wanawake.

Katika kusisitiza fursa hizo, Dk Biteko amesema  Tanzania Bara ina mawakili wa Serikali 785 na kati yao, wanawake ni 410 sawa na asilimia 52.

“Kwa upande wa Zanzibar, tuna jumla ya mawakili wa Serikali 76 na wanawake ni 34 sawa na asilimia 44 ya mawakili wote. Hivyo, ni muhimu kama nchi tujipongeze kwa kufikia hatua hii kubwa ya maendeleo na tunapozindua mpango kazi huu wa kitaifa wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, ni vyema tutambue kuwa, tayari tuna kitu cha kuanzia mkononi,” amesema Dk Biteko.

Ametoa rai kwa wizara zote zenye dhamana ya ajenda hiyo kwa Bara na Zanzibar, kuusimamia na kuutekeleza mpango huo kwa lengo la kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Waziri wa Maendela ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dorothy Gwajima ameelezea chimbuko la mpango kazi huo ambao kwa Tanzania mchakato wake ulianza mwaka 2020 kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Dk Gwajima amesema mpango kazi huo ni matokeo ya Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilielekeza kila nchi kuwa na mpango kazi wa kitaifa wa kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama

“Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana na kuja na azimio 1325 ambalo lilieleza kunapotokea changamoto na migogoro ya kiusalama wanawake,” amesema Dk Gwajima.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema wizara hiyo imeshiriki katika kila hatua kwenye mchakato wa kuandaa mpango kazi huo akibainisha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki kikamilifu kulinda amani.