Waandishi, wadau wa habari wamlilia Sharon, wamtaja mwalimu aliyeondoka

Dodoma. Mwandishi mwandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sharon Sauwa amefariki dunia.

Sharon amekutwa na umauti alfajiri leo Agosti 19, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Kifo chake kimepokewa kwa mshtuko na wanahabari wenzake na wadau wa habari, ambao wamemweleza kama mtu aliyekuwa mwalimu na kiongozi wa kipekee katika taaluma hiyo.

Sharon (50) kwa muda mrefu amekuwa mwandishi wa MCL (wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na Mwananchi Digital), akiwa amejiunga na kampuni Agosti 2013 akitokea The Guardian Limited, na kituo chake kilikuwa Dodoma.

Katika kipindi chote cha utumishi ameendelea kuwa nguzo na ametoa mchango katika idara ya habari ndani ya MCL kwa weledi na juhudi kubwa, hususan katika mikoa ya Dodoma na Singida.

Baba mzazi wa Sharon, Steven Lamlembe amesema mazishi ya mwanaye yatafanyika Alhamisi ya Agosti 21, 2025 katika makaburi ya Pugu Mwakanga jirani na Shule ya Sekondari ya Pugu, mkoani Dar es Salaam.

Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Joseph Damas amemwelezea Sharon kama mtu aliyeipenda kazi yake, msikivu, mwadilifu na aliyekuwa msaada mkubwa katika ukuaji wa wengine kutokana na kupenda ushirikiano.

Alisema wafanyakazi wa Mwananchi wamepokea msiba huo kwa mshtuko na masikitiko makubwa na kwamba, kifo chake kimekuwa cha ghafla.

Alisema kwa muda mrefu Sharon amekuwa kiunganishi na msaada mkubwa kwa wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wanaokwenda kuripoti habari za Bunge na kwamba, ndiye aliyekuwa kiunganishi pindi wanapohitaji msaada ikiwamo kuwapa miongozo na taratibu zinazopaswa kufuatwa.

“Ni msiba mzito kwa MCL na tasnia ya habari kwa ujumla, Sharon alikuwa mtu mwema na msaada mkubwa kwa wanahabari wanaokwenda kufanya kazi mkoani Dodoma hususan wakati wa vikao vya Bunge. Siku zote alikuwa mtu makini katika kusikiliza zaidi hoja na maelekezo, kutenda na kushauri pale inapofaa.

“Kifo chake kimeleta mshtuko na kuacha pigo kwa wafanyakazi wenzake hasa ikizingatiwa ameugua kwa muda mfupi sana. Daima tutakumbuka na kuyaenzi mazuri yake ikiwamo ukarimu, uchapakazi wake na moyo wa kuwasaidia wengine bila kujali,” amesema Damas. 

Waandishi wa habari na wadau wa habari wamemtaja Sharon kama nguzo na mwalimu kwa waandishi wanaochipukia, kutokana na ushirikiano aliokuwa nao nyakati zote kwenye masuala ya kitaaluma na hakuchoka kujifunza hata kwa waliochini yake.

Rafiki wa karibu wa Sharon, mwandishi wa magazeti ya Habari Leo, Annastazia Anyimike amemtaja kama mtu ambaye alikuwa kioo na msaada mkubwa kwa wenzake na aliyeishi kwa ushirikiano, bila kumbagua mkubwa wala mdogo na hakuangalia tofauti ya vipato vya watu.

Anyimike alisema yeye alimfanya Sharon kuwa mzazi wake na hivyo hivyo, mwenzake naye alijisikia vema kumuona Anyimike kama mzazi na mshauri wake wa karibu.

Alisema mbali na taaluma, waliweza kushirikishana mambo mengi, yakiwemo ya kifamilia.

“Binafsi alishakuwa zaidi ya ndugu na kwenye urafiki tulishatoka. Sharon ameniuma sana, sikutegemea kama ingekuwa rahisi hivi kwamba amepoteza maisha na siwezi kuongea naye tena kuanzia sasa, nimeumia sana na kweli ni kama siamini hiki kilichotokea,” alisema Anyimike.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dodoma, Mussa Yusufu amemtaja Sharon kuwa alikuwa kioo na mfano wa kuigwa hasa kwa waandishi wachanga, kwa kuwa wakati wote walimtumia kama darasa la wengine kujifunza kupitia maisha yake.

Mussa anasema ndani ya klabu hiyo Sharon alikuwa miongoni mwa waandishi wenye umri mkubwa na uzoefu kwenye tasnia kuliko walio wengi, hivyo alitumika kwa sehemu kubwa kutoa ushauri na kuwaelekeza kazi wenzake.

“Kwa watoto wa kike huyu alikuwa kama kungwi, tulimtumia kuwasaidia hata katika mazingira ya kawaida kutoa ushauri wa kimaisha na jinsi ya kusimama mbele ya viongozi, maana kizazi cha sasa kama unavyokijua huwezi kulinganaisha na watu wenye umri kama marehemu Sharon,” alisema Mussa.

Alisema alikuwa mwanachama mwaminifu ikiwamo kwenye ulipaji wa michango nyakati za matukio na ada za uanachama ndani ya umoja huo.

Kwa upande wake jirani na mmoja wa watu waliokuwa wakisali pamoja na Sharon, Zilipa Lyimo, alisema kifo hicho kimekuwa cha ghafla na kimewaumiza walio wengi, hasa waliokuwa wakisali pamoja.

Lyimo alisema kabla ya kifo chake, walimchagua kuwa mmoja wa viongozi katika jumuiya na kwamba alichaguliwa siku ambayo hata hakuwapo kwenye ibada, lakini kutokana na imani ambayo walikuwa nayo kwake, walimpa kura zote.

Akimzunguzia kwenye mtandao wa Instagram @berthMwambela ameandika: “Dada Sharon, asante kwa kuwa mwalimu mzuri kwetu. Nakumbuka nilipoanza kuandika taarifa za Bunge kwa mara ya kwanza ulinipa ushirikiano mzuri na kuniongoza vema. Asante kwa ukarimu na upendo wako. Tutaonana asubuhi iliyo njema lala salama.”

Naye Ummy Mwalimu, waziri wa zamani wa afya ameandika: “Ohh Noo! Hakika maisha ni safari. Pumzika kwa amani Sharon. Ulikuwa mwandishi mzuri mwenye uzoefu na weledi wa hali ya juu. Hakika ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari. Poleni @mwananchi_official.

“Binafsi pia nitakukumbuka kama mtu uliyependa na kujali afya yako. Nakumbuka mara kadhaa ambazo tulikuwa tunafanya pamoja mazoezi ya kutembea maeneo ya Mlimwa kwa Waziri Mkuu. Tulipeana moyo na kuhimizana kufanya mazoezi ya mara kwa mara! Pumzika kwa Amani Sharon. Mbele yako, Nyuma yetu. Pole kwa familia, ndugu na wote walioguswa na msiba huu.

Kwa upande wake @apema_anna alisema: “Jamani huyu dada daaah, apumzike kwa amani, alikuwa mtulivu mnooo “ Wakati @kulingemong.km aliandika: “RIP Sharon, unbelievable, go soon”.