Njombe. Wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, wametakiwa kufuata miongozo ya uendeshaji wa vituo hivyo kwa kuhakikisha kuwa vimesajiliwa na vina miundombinu bora kwa ajili ya usalama wa watoto.
Wito huo umetolewa leo Agosti 19, 2025 na Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo, Masinde Masinde wakati wa semina elekezi ya wamiliki wa vituo hivyo iliyofanyika wilayani Njombe.
Amesema wamiliki wa vituo hivyo wanatakiwa kuhakikisha wanafuata utaratibu uliotolewa na Serikali wa namna ya kuendesha vituo kwa kuwa na walimu wanaokidhi vigezo na mazingira rafiki kwa watoto.
Amesema uwepo wa miongozo hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na matukio mengine yasiyofaa kwenye jamii.
Amewataka wamiliki hao wa vituo kujenga vyoo bora, kuweka maji safi ya kunywa na kunawa mikono na kuhakikisha wanapima afya zao ili kuwalinda na magonjwa ya kuambukiza.
“Kitendo cha kufungua kituo bila ya kukisajili unaweza kuchukuliwa hatua za kisheria tunajitahidi sana kuelimisha ili tusifike huko” amesema Masinde.
Ofisa afya halmashauri ya mji wa Makambako, Neema Mollel amesema faini kwa wamiliki watakaoshindwa kutekeleza miongozo iliyopo ni Sh50,000 kwa kosa moja kwa mujibu wa sheria za ndani za halmashauri hiyo.
“Sheria ya halmashauri yetu kila kosa faini yake ni Sh50,000 mfano mpishi hajapima afya au hajavaa sare na makosa mengine akishindwa kutekeleza tunatumia sheria kubwa kosa ambapo faini ya kosa moja ni Sh1 milioni,” amesema Mollel.
Mwenyekiti wa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, Tulizo Fihanga amesema changamoto yao kubwa kwa sasa ni kukosa fedha ambazo zitawawezesha kuboresha kwa wakati mmoja vituo hivyo.
Ameahidi pamoja na changamoto hizo wapo tayari kufanyia kazi maagizo hayo ili kuimarisha ulinzi wa watoto katika vituo hivyo.
“Kama tutapata wadhamini au watu wa kutushika mkono na kuingia nao ubia nafikiri kwa namna moja au nyingine watakuwa wametusaidia,” amesema Fihanga.