Wazawa washirikiana na wageni kuleta neema ubanguaji korosho

Mtwara. Ili kufanikisha malengo ya kuongeza kiwango cha korosho kinachobanguliwa nchini Kampuni ya South Saharan Engineering Limited (SSEL) na Akros Limited kwa kushirikiana na wawekezaji wa kigeni wanatarajia kujenga kiwanda cha kuzalisha mashine za kubangua zao hilo.

SSEL inatarajia kushirikiana na kampuni ya JohnCashew Mashine kutoka nchini Vietnam, kiwanda kinatarajiwa kujengwa mkoani Mtwara eneo ambalo linaongoza kwa uzalishaji wa korosho hapa nchini.

Tanzania inalenga kukuza tija katika zao la korosho, miongoni mwa mipango yake ni kuzalisha na kubangua tani milioni moja ifikapo mwaka 2030. Kwa sasa wastani wa uzalishaji wa korosho ni tani 300,000, huku ubanguaji ukiwa ni asilimia chini ya 20.

Kuelekea malengo hayo, Tanzania imepanga kubangua tani 700,000 kufikia mwaka 2026, hata hivyo malengo yote hayo mawili yanahitaji juhudi za makusudi ili kuyafikia.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kwa wakulima wa korosho zaidi ya 300 mkoani Mtwara, Mkurugenzi wa Akros  Limited, John Joseph  amesema upatikanaji wa mashine hizo hapa nchini utaongeza kuliipa thamani zao hilo.

Joseph alisema kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake unatarajiwa kuwa zaidi ya Sh2.5 bilioni kitakuwa kinatengeneza mashine za kisasa ambapo zina uwezo wa kubangua kilo 600 kwa siku kwa mashine ya nyembe mbili, na kilo 1,800 kwa mashine  yenye nyembe nne.

“Malengo ya Serikali ni kuuza korosho zilizobanguliwa ifikapo 2030 yanaweza kutimia endapo kutakuwa na mashine za kisasa ili kuweza kuliongezea thamani ya zao hilo na kuwarahisishia wakulima kubangua korosho zao,” amesema Joseph.

Meneja wa viwanda vidogovidogo kutoka Mtwara, Zamla Dongwala  amesema wameona umuhimu wa kushirikiana na mwekezaji kutoka Vietnam kuanzisha karakana ya mashine za kisasa za kubangua korosho ili kuongeza  thamani zao hilo.

“Mashine zilizoletwa na mwekezaji huyo kutoka Vietnam zinaonyesha zitasaidia wabanguaji wadogowadogo wa zao la korosho kufanya kazi yao kwa haraka na kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali,” amesema Dongwala.

Akieleze kuhusu uwekezaji huo Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Alfred Francis amesema kuwa kiwanda kinachojengwa mkoani Mtwara eneo la Msijute kitasaidia wabanguaji  wa korosho kufanya kazi zao kwa haraka, kwani mashine zitakazotengenezwa ni za kisasa.

“Nimshukuru mwekezaji huyu kwa kuleta ujenzi wa kiwanda mkoani Mtwara, kitakachosaidia kuongeza thamani ya zao letu na malengo yetu kama nchi ifikapo 2030 tutaweza kuzalisha korosho tani milioni 1 na kuuza korosho zote zilizobanguliwa,” amesema Francis.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya ameitaka bodi ya korosho kuendelea kuhamasisha wadau  kuanzisha viwanda vidogovidogo vya ubanguaji wa korosho, huku wakiendelea kusubiri kiwanda kinachojengwa.

Mbanguaji wa korosho kutoka Tandahimba, Mariam Saidi, amesema kuwa ujio wa kiwanda hicho utasaidia kuongeza uchumi wa nchi kwani watafanya kazi hiyo bila kuchoka.