Aliyehukumiwa kwa kujifanya usalama wa Taifa aachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya, imemuachia huru George Mwakifamba, aliyekuwa amekutwa na hatia katika makosa sita ikiwemo kujifanya ofisa usalama wa Taifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, utekaji nyara na kutishia kwa lengo la kujipatia Sh20 milioni.

Mrufani huyo na wenzake wawili (siyo warufani katika rufaa hiyo) ambao ni Deodatus Patrick na aliyekuwa Ofisa wa Jeshi la Polisi, Koplo Erica John, walishtakiwa kwa pamoja katika makosa sita na kukutwa na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo na faini.

Hukumu hiyo imetolewa Agosti 18, 2025 na Jaji Victoria Nongwa aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai ambapo baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa na hoja za pande zote mbili, alikubaliana na rufaa na kufuta hukumu iliyokuwa imetolewa dhidi yake.

Mrufani na Deodatus, alikuwa anakabiliwa na makosa ya kujifanya ofisa wa umma, kinyume na kifungu cha 100(b) cha Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa Mei 3, 2024 eneo la Kasumula wilayani Kyela mkoani Mbeya kwa pamoja na washtakiwa hao kwa pamoja walijiwakilisha kwa uongo kuwa wao ni maofisa usalama wa Serikali kwa Edward Rugela na Mei 4, 2024 kwa Aman Thomas jambo ambalo walilijua kuwa ni la uongo.

Kosa la tatu na lililokuwa likiwakabili wote watatu lilikuwa ni kudai fedha kwa vitisho kinyume na kifungu cha 292 cha Kanuni ya Adhabu ambapo Mei 3, 2024 walidaiwa kwa nia ya kuiba walidai Sh20 milioni kwa vitisho kutoka kwa Tumaini na Aman kwenda kuwaombea ofisini kwa Waziri Mkuu Dodoma.

Kosa la tano na sita kwa washtakiwa wote lilikuwa ni utekaji nyara kinyume na kifungu cha 246 na 35 cha Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa Mei 3, 2024 eneo la Kasumula wilayani Kyela mkoani Mbeya kwa pamoja na washtakiwa walitumia nguvu kuwalazimisha Tumaini na Aman kwenda kuhojiwa Dodoma jambo ambalo walilijua kuwa ni la uongo, makosa ambayo washtakiwa wote waliyakana.

Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na  mashahidi tisa na vielelezo vitano huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi watano.

Shahidi wa tatu, (Tumaini), alidai siku ya tukio saa mbili usiku wanaume wawili walimfuata na kujitambulisha ni maofisa usalama kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma na kumweka chini ya ulinzi, na kumtaka kusalimisha kila alichokuwa nacho.

Alidai gari lilifika na kulazimishwa kuingia ndani, alikuta watu wengine watatu na mmoja alikuwa mwanamke aliyevaa sare za polisi na kuambiwa wanaelekea Dodoma, aliomba kuwajulisha ndugu na jamaa lakini akakataliwa.

Shahidi huyo alidai aliomba aelezwe alichofanya bila mafanikio, ambapo alitishiwa kueleza kila kitu kingine angeuawa, lakini walikuwa tayari kumsaidia.

Alidai kuwa watu hao walidai Sh20 milioni ili wamwachie na aliwasiliana na jirani yake ili auze gari lake, mke mkubwa upendo ili kuweka nyumba rehani na mke mdogo ambaye alimtumia Sh1 milioni na walipofika Uyole walikwenda kituo cha mafuta na akalipa Sh150,000  na kwa wakala wa fedha kutoa Sh850,000 alizompa mrufani.

Aliieleza Mahakama kuwa mkewe (Upendo) alipata mteja wa nyumba hiyo na wakaanza safari ya kurudi Kasumulu kusaini makubaliano ambapo walisimama kwenye baa ya G8 na mtu mwingine Aman aliletwa.

Shahidi wa nne (Aman), alidai kukamatwa Mei 4, 2024 na watu wawili waliojitambulisha ni maofisa usalama kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, alipandishwa kwenye gari na kuanza safari ya kuelekea Dodoma.

Alidai alipouliza kuhusu makosa yake alivamiwa na kutishiwa na watu hao walimdai Sh20 milioni ili kumsaidia, ambapo alimpigia rafiki yake ili atafute fedha hizo.

Kuhusu mtego namna walivyokamatwa, shahidi wa pili alidai kupokea simu kutoka kwa shahidi wa tano, Musa Kavina ambapo walijulishwa Aman alikamatwa na baadhi ya watu waliomtambulisha kuwa ofisa usalama kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma na walikuwa wakimpeleka Dodoma.

Alidai kutumiwa namba za usajili wa gari hilo na kuweka mtego Makasini Uyole, gari hilo lilikuwa na watu watano na mmoja wao alikimbia na waliobaki ni mrufani na mshitakiwa wa pili pamoja na shahidi wa tatu na wa nne.

Katika utetezi mrufani alikana kutenda kosa hilo, alieleza kuwa shahidi wa tatu na nne walimpatia risiti bandia kwa ajili ya kusafirisha mizigo yake kwenda Rwanda na kuwa na gari hilo lilikamatwa Makambako na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na kuripoti Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Alidai kuwa TRA walimwambia atafute mtu aliyempa risiti hiyo ambapo Mei 4, 2024 alienda Kyela kumpeleka Aman TRA Makambako.

Ushahidi huo uliungwa mkono na Venance Azigard (shahidi wa nne wa utetezi) ambaye alidai siku hiyo gari la mrufani lilikamatwa kwa sababu alikutwa na risiti bandia na kuwa aliombwa kutoa ushirikiano wa kuwatafuta wahusika waliotoa risiti hiyo na baadaye aliitwa kuhojiwa Takukuru.

Baada ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo wote watatu akiwemo mrufani walikutwa na hatia ambapo kosa la kwanza na la pili mrufani alihukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au jela miaka miwili.

Kosa la tatu na nne, kifungo cha miaka minne na kosa la tano na sita faini ya Sh1 milioni au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.

Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo, mrufani alikata rufaa Mahakama Kuu akiwa na sababu nane ikiwemo hakimu alikosea kumtia hatiani na kumuhukumu kwa kuzingatia shitaka lenye dosari isiyoweza kutibika.

Hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani na kumuhukumu mrufani kwa kosa la utekaji nyara, na hivyo kutoa msingi wa kutiwa hatiani kwa ufafanuzi tu wa kosa ambao haukuwa unaonyesha vipengele muhimu vya kosa, makosa hayakuthibitishwa.

Sababu nyingine ni Hakimu alikosea kisheria  kwa kushindwa kuchambua, kutathmini na kuzingatia utetezi wa mrufani na kuwa ushahidi wa makosa hayo ulikuwa dhaifu, usio na uwiano na unaokinzana.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mrufani aliwakilishwa na Wakili Freius Kakulima huku mjibu rufaa akiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Rajabu Msemo.

Kuhusu kosa la utekaji nyara, alidai kuwa kifungu cha 246 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu hakijengi kosa hilo kwa kuwa hakuna vipengele muhimu vya kosa lililoelezwa.

Kuhusu kosa la kwanza na la pili, alieleza kuwa kulikuwa na dosari katika shtaka hilo, hivyo kukiuka kifungu cha 132 na 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na kuwa dosari hiyo haiwezi kutibika chini ya kifungu cha 411 cha CPA kwa kuwa haikufichua kosa lolote linalojulikana.

Wakili huyo alidai makosa ya kujifanya ofisa wa umma na utekaji nyara hayakuthibitishwa bila shaka.

Jaji Nongwa amesema baada ya kusikiliza uwasilishwaji wa sababu za rufaa na mwenendo wa shauri hilo, masuala mawili yanayobika ni iwapo makosa ya utekaji nyara yalifichua kuwa mrufani ni miongoni mwa wanaume waliojitambulisha kuwa maofisa usalama au waliokutwa kwenye gari.

“Kuhusu kosa la utekaji nyara, kutokana na uwasilishaji wa wapinzani, ni wazi kuwa kutaja kifungu cha 246 hakikuwa sahihi na dosari haiwezi kutibika  kutokana na kifungu kinachorejelewa kuunda kosa tofauti ambalo kama ilivyokubaliwa na wakili wa Serikali halikutajwa katika taarifa ya kosa hivyo mrufani alitiwa hatiani kimakosa.”

Kuhusu iwapo upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila shaka yoyote, Jaji alianza kwa makosa ya kudai fedha kwa vitisho chini ya kifungu cha 292 cha kanuni ya adhabu na kuwa ili kuthibitisha kosa hilo vipengele vitatu lazima viwepo ikiwemo matumizi ya vitisho.

Jaji Nongwa baada ya kupitia sababu zote, alikubaliana na rufaa hiyo kutokana na makosa hayo kutothibitishwa hivyo kufuta adhabu na kuiweka kando katika makosa yote na kuamuru mrufani achiwe huru.