Dar es Salaam. Licha ya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha biashara, tathmini inaonyesha asilimia 17.1 ya nguvu kazi ya jiji hilo haitumiki kwa sababu ya kukosa shughuli za kufanya.
Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi 2022, ambazo zinaonyesha wanawake ndio wanaongoza kwenye kundi hilo la nguvu kazi isiyotumika.
Kwa sasa Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na wakazi milioni 5.7 kati ya hao, nguvu kazi ni milioni 3.2. Kwa mujibu wa makadirio hayo, jumla ya watu 548,000 (sawa na asilimia 17.1 ya nguvu kazi) hawafanyi kazi.
Wakati takwimu zikionyesha hivyo, jiji hilo linaoongoza kwenye orodha ya mikoa yenye idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), hivyo kushindwa kwao kufanya kazi hakuna uhusiano wa moja kwa moja na kukosa stadi za KKK.
Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 2.5 pekee ya wakazi wa jiji hilo ndiyo hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu, na hivyo kuufanya mkoa kinara wenye idadi kubwa ya watu wenye stadi za KKK.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Profesa Philipo Sanga akizungumza wakati wa mafunzo ya ujasiriamali kwa mamalishe.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Profesa Philipo Sanga wakati wa mafunzo ya ujasiriamali kwa mamalishe wa jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo.
Amesema jiji hilo lina watu wengi wenye elimu, lakini wapo wanaoshindwa kuitumia vyema kujiajiri na badala yake wanaishia kulalamika kuwa hakuna ajira.
Profesa Sanga amebainisha kuwa asilimia 21.6 ya wanawake katika jiji hilo hawana shughuli za kufanya, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya kazi huku wanaume katika kundi hilo wakiwa asilimia 12.6.
Kufuatia hilo, TEWW imetoa mafunzo maalumu kwa wanawake wanaojihusisha na biashara ya chakula maarufu kama mamalishe ili kuwapa elimu ya ujasiriamali kuwaimarisha kwenye biashara hiyo.
“Tunafahamu kuishi katika mkoa huu inahitaji akili sana, ndiyo maana taasisi ya elimu ya watu wazima tunatoa elimu itakayowawezesha kupata stadi mbalimbali zitakazowawezesha kujiajiri.
“Tumefanya hivyo kwa makundi ya bodaboda, mamalishe ili kutoa hamasa kwa wengine waone kwamba shughuli hizo na zinazofanana na hizo, zinaweza kuwa ajira kwao na kujiondoa kwenye kundi la watu wenye nguvu kazi isiyotumika,” amesema Profesa Sanga.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kutotumika kwa nguvu kazi ni matokeo ya watu kutoziangalia changamoto kama fursa.
“Ukiziangalia changamoto kama changamoto unaweza kusema huna cha kufanya, lakini ukiziangalia kama fursa utapata cha kufanya, mfano tunaona takataka ni changamoto lakini katika mataifa mengine takataka ni chanzo cha ajira.
Watu wasipuuze maarifa yanatotokana na elimu ya watu wazima ili waone ni namna gani wanaweza kuyatumia. Pia, Dar tumebahatika kuwa na makundi mbalimbali ya watu, hii ni fursa ya wewe usiye na cha kufanya kujifunza kwa wale wanaofanya,” amesema.
Kuhusu elimu ya watu wazima, Chalamila amesema ni eneo linalohitaji kupewa kipaumbele hasa katika karne ya sasa, kwani kupitia elimu hii, mamalishe naye pia huweza kunufaika na ujuzi sambamba na kupata stadi za KKK.
Amesema Serikali imeendelea kutambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika ukuzaji wa pato laTaifa mama Lishe wakiwa sehemu ya watoa huduma muhimu, ambayo huchangia pato hili.
“Hata hivyo, kwa upande wenu mamalishe, masuala ya usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo mnayofanya shughuli zenu, bado yana changamoto za kutozingatia usafi na utunzaji wa mazingira.
“Ni muhimu kuzingatia suala zima la usafi wa mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi watusaidie kuepukana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati zisizo salama, kama vile kuni ambazo zinazotengeneza moshi mzito ambao hatimaye unaweza kusababisha magonjwa ya kifua.