Aucho kimeeleweka Singida Black Stars

SINGIDA Black Stars imekamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo wa Yanga, Khalid Aucho ikimpa mkataba wa miaka miwili.

Mwanaspoti lilisharipoti uwepo wa mazungumzo ya Singida Black Stars kumnasa kiungo huyo raia wa Uganda na sasa ni rasmi amemwaga wino huku muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa rasmi tayari kwa maandalizi ya msimu wa 2025/26.

Chanzo cha kuaminika kutoka Singida Black Stars, kililiambia Mwanaspoti  tayari wamemnasa kiungo huyo kwa mkataba wa miaka miwili na atakuwa sehemu ya malengo yao msimu huu ndani na kimataifa.

“Tulipokuwa tunauza wachezaji tulikuwa na mipango mingine mikubwa ambayo siku ya Singida Big Day ndiyo tutatoa majibu kuwa bado tutakuwa na timu bora na ya ushindani, sio Aucho tu, kuna nyota wengine bora,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.

“Tuna malengo makubwa, kinachozingatiwa sasa ni uzoefu na ubora, kila mmoja anafahamu ubora wa Aucho akifanya mambo makubwa kwenye ligi yetu, tunaamini atafanya hivyo pia akiwa Singida Black Stars.”

Alisema wamefanya uamuzi wa kumnasa kiungo huyo kutokana na uzoefu na ubora alionao huku wakiamini atakuwa mchezaji kiongozi katika timu yao kutokana na kuwa na uzoefu wa ndani na kimataifa.

Aucho anaifahamu vizuri Ligi ya Bara kutokana na kuichezea Yanga misimu minne tangu alipojiunga nayo Agosti 2021, akitokea Misr Lel Makkasa SC ya Misri na kuondoka mwisho wa msimu wa 2024-2025 na muda wote huo amekuwa kiungo namba moja na mchezaji wa kutumainiwa eneo la ukabaji.

2009–2010 Jinja Municipal

2018–2019 Churchill Brothers