Chaumma kijielekeze kuikabili CCM uchaguzi mkuu 2025

Mtiania wa urais wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, anazunguka kutafuta wadhamini.

Anatumia jina la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujinadi.

Salum, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, Zanzibar, jukwaa kwa jukwaa, chama chake cha zamani hakikauki mdomoni. Ajabu, Chadema hawashiriki Uchaguzi Mkuu 2025, hivyo si washindani wa Chaumma. Kwa sasa, Salum ni Katibu Mkuu Chadema.

Uchaguzi Mkuu 2020, Salum alikuwa mgombea mwenza wa urais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akichangia tiketi ya Chadema na Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, ambaye wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara. Lissu ndiye hasa alikuwa mgombea urais.

Salum, anatumia historia hiyo ya kuwa mgombea mwenza kupitia Chadema kuomba kuungwa mkono ngazi ya urais akipeperusha bendera ya Chaumma. Salum anasema, kama aliaminiwa umakamu wa rais, basi aaminiwe urais.

Kabla ya hapo, Salum alizunguka akisema kuwa muda ungefika, Chadema wangeomba kuketi meza moja na Chaumma kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, utakaofanyika Oktoba 29, 2025. Si Salum tu, viongozi karibu wote wa Chaumma, jina la Chadema limejaa kwenye ulimi kila wanapokuwa majukwaani au katika mazungumzo na waandishi wa habari.

Ni kweli, hata viongozi wa Chadema wamekuwa wakiwashambulia wenzao waliojiunga na Chaumma. Msingi wa hoja ninaouombea ufahamu ni kwamba Chadema hawashiriki uchaguzi, kwa hiyo Chaumma wanapaswa kushindana na vyama vinavyoshiriki, hasa CCM wanaoshika dola.

Nafahamu, Chaumma wapo kwenye mapambano ya kuufanya umma uone ilikuwa halali kwao kuondoka Chadema, kisha kutafuta jukwaa la tofauti la kufanyia siasa. Pamoja na hivyo, muda uliobaki kufikia Uchaguzi Mkuu ni miezi miwili, Chaumma wanatakiwa kujikita kupambana na washindani wao wa kweli. Wangeachana na Chadema.

Chaumma wanapaswa kuuangukia umma, ujue umuhimu wao wa kushiriki Uchaguzi Mkuu, vilevile wanadi sera zao ili kulifanya taifa lione ni kwa nini wao wanafaa na siyo CCM waliopo madarakani. Wawathibitishe na wawanadi viongozi wao ili kuonesha kwamba wana sifa za uongozi na maarifa ya kiuongozi kuliko wa vyama vingine.

Itakapofika siku ya kupiga kura, karatasi ya mpigakura haitakuwa na mgombea yeyote wa Chadema. Kwa mantiki hiyo, ni kupoteza muda kushindana na watu ambao hawatakuwa kwenye karatasi ya kuchagulia viongozi siku ya uchaguzi. Chadema wamekuwa wakiisema Chaumma kwamba ni mradi wa CCM ili kukidhoofisha chama chao. Kitendo cha Chaumma kuitumia zaidi Chadema majukwaani, inarahisisha nguvu ya hoja za chama hicho dhidi yao. Hawapaswi kukubali hili.

Chaumma, wangepaswa kuitaja Chadema nyakati tu za kufafanua ulazima wao wa kuachana na chao cha zamani na kusuka jukwaa jipya ndani ya Chaumma. Baada ya hapo, washughulike na CCM, ambao ndiyo wenye dola. Mwisho kabisa, matamanio ya chama cha upinzani ni kushika dola.

Chadema wao wameshika msimamo wa No Reforms, No Election, kwamba bila mabadiliko ya kimsingi katika sheria za uchaguzi, hawashiriki uchaguzi. Msimamo huo ndiyo ambao umesababisha chama hicho kiwe nje ya mchakato wa kuelekea Oktoba 29, 2025.

Kuna makosa pia kwa Chadema kujielekeza kupambana na vyama vingine vya upinzani, badala ya kuweka mkazo ili Watanzania wengi waelewe kwa nini ni muhimu uchaguzi kutofanyika mpaka kwanza mabadiliko yafanyike. Chaumma na ACT-Wazalendo, ni waathirika wa mashambulizi ya Chadema.

Hata hivyo, kinachotakiwa kwa Chaumma, kama ilivyo ACT-Wazalendo, ni kujikita kwenye uchaguzi. Haiwezekani imebaki miezi miwili na siku tisa, huchangi karata zako vyema kuelekea uchaguzi, badala unashughulika zaidi na makundi ambayo si sehemu ya ushindani.

Naelewa, Chadema wangependa kuona vyama vya upinzani, hasa ACT-Wazalendo na Chaumma, wanakutana na cha mtema kuni kwenye uchaguzi, ili wathibitishe uhalali wao wa kutoshiriki uchaguzi.

Vyama vya upinzani ambavyo vimeridhia kushiriki uchaguzi, vinatakiwa vijikite kuukabili uchaguzi ipasavyo ili vihalalishe ushiriki wao kwenye uchaguzi.

Matokeo ndiyo yatathibitisha. Chaumma na ACT-Wazalendo, wakipata viti vya ubunge na madiwani, watapata nguvu ya kuuambia umma ni kwa nini ilikuwa uamuzi wa busara kwao kushiriki uchaguzi.

Chadema watathibitisha kwa jumuiya kwamba walikuwa sahihi, kama vyama vya upinzani vitatoka na vilio vya kuibiwa kura au kupokwa ushindi. Chaumma watambue kwamba mpinzani wao ni CCM. Wajikite kufafanua udhaifu wa chama hicho. Maeneo waliyoshindwa kupeleka maendeleo, nao wajinasibu ni kwa namna gani siku wakipata nafasi mambo yatabadilika kwa ubora. Chama chao cha zamani hakipaswi kuwa sera yao ya kudumu.

Salum kutumia Uchaguzi Mkuu 2020 ni shabaha ndogo. Vipimo vingi vimeonesha kuwa ulikuwa uchaguzi ulioharibiwa zaidi katika historia ya Tanzania. Na kwa kuuendea kwenye matokeo, Chadema walipata anguko kubwa. Salum anasema “aliaminiwa” 2020, anatumia vigezo gani?

Kama tiketi aliyopewa na Chadema ndiyo imani anayomaanisha, maana yake shabaha yake ni ndogo. Anapaswa kuzungumza na nchi kuhusu anayotarajia kuyafanya akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo CCM wameshindwa au hawataweza.

Kilichopo sasa ni dhahiri kwamba Chaumma wameingia kwenye uchaguzi wakiwa hawatambui nani hasa ndiye msindani wao wa kisiasa.

Lazima wawe na shabaha moja ili kuwafanya wananchi wawaamini. Hawapaswi kuwa na agenda za kurukaruka. Hawatakiwi kushindana na timu isiyoshiriki ligi.

Kwa sasa, ligi ya kisiasa iliyopo ni Uchaguzi Mkuu 2025. Timu zinazoshiriki ligi zinafahamika, kwa hiyo Chaumma wajikite nazo. Chaumma wakwepe kushughulika na Chadema ili kujiweka kando na tuhuma kuwa wao (Chaumma) ni mradi wa kuhakikisha chama hicho kinadhoofika, na si kweli wanajipanga kushinda na CCM kwenye uchaguzi.