Ikulu ya Marekani yazindua akaunti ya Tiktok licha ya zuio la Trump

Marekani. Ikulu ya Marekani imezindua akaunti rasmi kwenye TikTok inayomilikiwa na Wachina ikiwa bado mwezi mmoja kuanza utekelezaji wa ahizo la Rais Trump kupiga marufuku jukwaa hilo la mitandao ya kijamii kutumika nchini Marekani.

Sheria ya ulinzi wa data ya mwaka 2024 ilihitaji TikTok kusitisha shughuli zake ifikapo Januari 19 mwaka huu isipokuwa kama ByteDance, kampuni mama ya programu hiyo, ingepata leseni ya uendeshaji wake wa Marekani.

Trump, ambaye alikuwa mtumiaji mkubwa wa TikTok wakati wa kampeni zake za urais, aliongeza muda wa mwisho hadi mapema Aprili, kisha Juni 19 na kuwapa muda hadi Septemba 17.

Akaunti hiyo ya @WhiteHouse tayari imepata zaidi ya wafuasi 80,000 tangu izinduliwe jana Jumanne kupitia video fupi iliyomwonyesha Rais na maandishi yaliyosomeka: “America we are Back! What’s up TikTok?”

Awali Rais Trump alitahadharisha kuwa kusambaa kwa TikTok kuwa ni “Janga la kitaifa” aliposaini agizo la kiutendaji mwaka 2020 lililoweka vikwazo vingi dhidi ya programu hiyo wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais.

Trump alisema ukusanyaji data wa programu hiyo “Unatishia kutoa fursa kwa Chama cha Kikomunisti cha China kupata taarifa binafsi na za siri za Wamarekani jambo linaloweza kuruhusu China kufuatilia maeneo ya wafanyakazi wa serikali ya shirikisho.”

Alikosoa pia madai ya TikTok ya kuficha maudhui nyeti kisiasa kuhusu maandamano ya Hong Kong na namna China inavyowatendea Wauyghur na makundi mengine.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi mpya wa Ikulu wa kutumia jukwaa hilo, Katibu wa Habari Karoline Leavitt amesema: “Ujumbe wa Rais Trump ulitawala TikTok wakati wa kampeni yake ya urais, na tunafurahia kujenga juu ya mafanikio hayo na kuwasiliana kwa njia ambayo hakuna utawala mwingine umewahi kufanya.”

Akaunti binafsi ya TikTok ya Rais Trump @realdonaldtrump imekuwa hai tangu Juni 2024 na tayari ina zaidi ya wafuasi milioni 15.