Agosti 18, 2025, Jaji Mutungi alifungua mafunzo kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa jijini Dar es Salaam yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere.
Mafunzo hayo yaliwaleta pamoja viongozi na wadau wa siasa kujadili kwa kina Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Lengo lilikuwa kuongeza uelewa wa namna sheria hiyo inavyotekelezwa ili kuepuka dosari wakati wa kampeni na uchaguzi mkuu ujao. “Tunapaswa kuzingatia Sheria za nchi, katiba za vyama vyetu na miongozo ya Baraza la Vyama vya Siasa ili kuepusha migogoro,” alisisitiza Jaji Mutungi.
Sheria hii ni chombo muhimu katika siasa za kidemokrasia kwa kuwa inalenga kuhakikisha kila mgombea anapata nafasi ya kushindana kwa haki, bila kulazimishwa kushindana kwa nguvu ya pesa.
Kupitia utekelezaji wake, wagombea hupatiwa fomu za matumizi ya fedha, wanatakiwa kuzijaza na kurudisha kwa wakati, huku mienendo yao ikifuatiliwa kwa karibu.
Hatua hii husaidia kudhibiti vitendo haramu kama rushwa ya kisiasa na matumizi ya mali za umma kwa manufaa ya kisiasa.
Mkutano huu ulikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa moja ya majukumu saba makuu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Majukumu hayo ni pamoja kusimamia mapato na matumizi ya vyama vya siasa wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2010.
Kusajili na kufuta vyama vinavyokiuka masharti ya usajili kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 na kuratibu shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa.
Kufuatilia utendaji wa vyama ili viende sambamba na sheria, kugawa ruzuku kwa vyama vyenye sifa sambamba na kuwa kiunganishi kati ya serikali na vyama vya siasa pamoja na kutoa elimu kwa umma na wadau wa siasa.
Kwa kuzingatia majukumu haya, Ofisi ya Msajili imekuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha vyama vinaheshimu misingi ya sheria na taratibu za kidemokrasia.
Kwa mantiki hiyo, Jaji Mutungi amewasisitiza viongozi wa siasa kuzingatia katiba na sheria za nchi pamoja na miongozo ya vyama vyao ili kuepuka migongano ya mamlaka na migogoro ya kisiasa.
Vilevile, amekumbusha kuwa hata wanachama wa vyama wana wajibu wa kuheshimu katiba na kanuni, ndani na nje ya chama, kwa lengo la kujenga umoja na maendeleo. Maneno yake yalikuwa wazi: “Mzingatie Sheria za nchi, mzingatie katiba za vyama vyenu na sheria zinazoratibiwa na Baraza la Vyama vya Siasa.”
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Ofisi ya Msajili, Muhidin Mapejo, Sheria ya Gharama za Uchaguzi imeweka viwango vya juu vya matumizi ya fedha kwa wagombea.
Amesema mgombea urais si zaidi ya Sh9 bilioni, mgombea ubunge kiwango kimepangwa kulingana na idadi ya watu, ukubwa wa eneo na hali ya miundombinu ya jimbo, ambapo kiwango cha juu Sh136 milioni na mgombea udiwani matumizi yake yasizidi Sh16 milioni.
Hata hivyo, kwa mtazamo binafsi, viwango hivi vinaonekana kuwa vidogo na vimepitwa na wakati, hasa tukizingatia gharama halisi za kampeni katika mazingira ya sasa. Changamoto kubwa inayojitokeza ni lugha inayotumika kwenye sheria na fomu zinazohusu uchaguzi, ambazo zote zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Wakati sifa ya msingi ya kugombea ni kujua kusoma na kuandika, wagombea wengi wa elimu ya msingi au sekondari ya kawaida hujikuta hawawezi kuelewa maelezo hayo.
Hali hii husababisha vyama vikubwa, hasa chama tawala, kuwasaidia wagombea wao kwa kujaza fomu, huku wapinzani wakishindwa na mara nyingi kuenguliwa.
Hatua ya Msajili kuandaa mafunzo kwa viongozi wa vyama ni muhimu, kwa sababu ikitokea mgombea anaenguliwa safari hii, itakuwa ni kutokana na kutozingatia elimu waliyopatiwa.
Zaidi ya hapo, siasa za Tanzania zimekuwa zikielekezwa na fedha. Vyama vinapokusanya fedha, mara nyingine huchangisha kiwango kinachozidi viwango vilivyowekwa kisheria. Tumeona mfano, fedha zinazokusanywa hufikia hadi Sh 100 bilioni, wakati sheria inaruhusu chini ya bilioni 10 kwa urais.
Hii inaleta taswira kwamba siasa zetu zimegeuka kuwa za kifedha zaidi kuliko za sera na uongozi.
Kwa lugha ya mitaani, “pesa ndefu ndiyo kisu kikali,” na mwenye kisu hukata nyama. Hali hii inawanyima nafasi viongozi bora wasiokuwa na uwezo mkubwa kifedha. Ni muhimu kutambua kwamba siasa si suala la fedha pekee. Vyama na wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kutazama uwezo na maono ya kiongozi badala ya kufuata ukubwa wa mfuko wake.
Wananchi wanapaswa kuwa makini, wakiletewa zawadi, fulana, kofia, khanga au hata chakula wakati wa kampeni, wakipokee kama sehemu ya haki yao, lakini siku ya kupiga kura wachague kiongozi mwenye uwezo wa kuleta maendeleo, hata kama hana fedha nyingi.
Uongozi bora haupimwi kwa kiasi cha fedha kilichotumika kushinda uchaguzi, bali kwa uwezo wa kiongozi kutatua changamoto za wananchi na kusimamia maendeleo ya taifa. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inastahili pongezi kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kwa kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wadau wa kisiasa.
Mwisho wa yote, wananchi wanapaswa kukumbuka kuwa kura yao ndiyo silaha kubwa. Tuchague viongozi, si pesa.