BAADA ya kufuzu hatua ya robo fainali timu ya taifa ya Sudan imeonekana kuingia kwenye hali ya kujiamini, kutokana na kocha Kwesi Appiah kuwapongeza wachezaji wake akidai kwamba wamekuwa wakibadilika mechi hadi mechi kuonyesha ubora.
Sudan imefuzu hatua hiyo baada ya suluhu dhidi ya mabingwa wa michuano ya CHAN, Senegal na kufanikiwa kuongoza kundi D ikiwa na pointi tano sawa na Senegal iliyopo nafasi ya pili tofauti ni mabao ya kufunga na kufungwa.
Appiah alisema kuwa tofauti kubwa imeonyeshwa na wachezaji wake akiisifia safu ya ulinzi kufanikiwa kuwadhibiti mabingwa watetezi wa michuano hiyo na kuonyesha mchezo mzuri wa ushindani.
“Senegal ni bingwa mtetezi, nawapongeza wachezaji wangu kwa kucheza mchezo mzuri na kutotoa nafasi ya kuadhibiwa mbele ya timu bingwa na bora. Haikuwa rahisi, lakini najivunia timu yangu ilianza vibaya michuano na kadri inavyopata mechi inazidi kuimarika,” alisema na kuongeza:
“Tulipata nafasi nyingi za wazi tulishindwa kuzitumia siyo kwamba ni udhaifu bali ni sehemu ya mchezo na unatakiwa kuzingatia tumecheza na timu ya aina gani. Kwa sasa matokeo hayo tumeyasahau tunazingatia maandalizi kwa ajili ya mchezo wa robo fainali.”
Kocha huyo alisema mbinu waliyotumia ya kujilinda dhidi ya mabingwa hao bila ukuta imara wasingeweza kufanikiwa na kwamba walifanya kazi zote kwa wakati mmoja – kujilinda na kujaribu kutafuta bao la kuongoza, lakini haikuwa bahati kushinda, ila wanashukuru wemepata nafasi ya kutinga hatua ya robo wanakoenda kushindana.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Sudan kuendelea kuwa pamoja na timu kwa kuipa sapoti katika maombi akisisitiza kuwa peke yao hawawezi wanahitaji sapoti na wao wanaahidi kuto kuwaangusha.
Katika mechi mbili za awali, Sudan imeonyesha kiwango kizuri kwenye kujilinda, timu hiyo imeruhusu bao moja tu, lililofungwa na Congo katika mechi ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya 1-1 huku ikiwa ndio timu iliyofunga mabao mengi kundi D.