‘Mabosi’ walioshikilia hatima ya urais 2025

Dar es Salaam. Siri ya ushindi wa kiti cha urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, imejificha katika mikoa 10, ukiwamo Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Tabora, Kagera na Geita.

Ingawa ushindi katika uchaguzi, unabebwa na makusanyo ya kura kutoka maeneo mbalimbali, mikoa hiyo inaonyesha kuwa na nguvu ya kuamua mshindi wa kiti cha urais.

Hilo linatokana na ukweli kwamba, mikoa hiyo ndiyo vinara kwa wingi wa wapigakura kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ukilinganisha na mingine.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Tabora, Kagera, Dodoma, Tanga, Geita, Arusha na Mbeya, ikijumuisha asilimia 53.73 ya wapigakura wote nchini.

Mathalan, katika jumla ya wapigakura milioni 37.65 wa Tanzania, Mkoa wa Dar es Salaam pekee, wapo milioni 4.4 sawa na asilimia 11.74.

Mkoa wa Mwanza ni asilimia 6.02, Morogoro (5.61), Tabora (4.78), Kagera (4.68), Dodoma (4.64), Tanga (4.34), Geita (4.07), Arusha (4.06) na Mbeya (3.79).

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya siasa, wanasema pamoja na wingi wa wapigakura katika mikoa hiyo, mwamko wao wa kujitokeza kwenda kushiriki upigaji kura ndiyo utakaoamua mshindi.

Mtazamo huo wa wadau, unabebwa na uhalisia wa kihistoria. Katika uchaguzi kama huo uliofanyika mwaka 2020, jumla ya wapigakura 29,754,699 waliandikishwa. Kati yao ni 14,662,746 hawakujitokeza kupiga kura, sawa na asilimia 49.27.

Hata hivyo, idadi hiyo ilikuwa chini zaidi ya ile ya waliojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo asilimia 67.34 ndiyo waliojitokeza.

Kuhusu hoja hiyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha (Udom), Dk Paul Loisulie anasema majimbo na mikoa kuwa na idadi kubwa ya wapigakura isiwe na maana zaidi wakati wa kampeni kwa sababu huenda watu hao wasijitokeze.

Pamoja na hayo, anasema ni muhimu wanasiasa wanaogombea urais kuyawekea macho maeneo hayo kwa lengo la kutafuta kura.

“Maeneo yenye wapigakura wengi yanaweza kuamua matokeo ya urais, nguvu kubwa ikielekezwa kwenye maeneo hayo vyama vitanufaika na wingi wa kura,” anasema.

Dk Loisulie anasema wagombea wa nafasi za juu maeneo kama hayo ndiyo fursa yao kutumia takwimu hizo kuangalia maeneo gani wanayokubalika ili kuweka nguvu wakati wa kampeni.

Dar es Salaam mwaka 2020, ulisajili zaidi ya wapigakura milioni 3.1, sawa na zaidi ya asilimia 10 ya wapiga kura wote nchini. Hii ni turufu isiyoepukika, kwa sababu si tu kitovu cha biashara, bali pia ni mchanganyiko wa tabaka na makundi ya kijamii wenye mitazamo tofauti ya kisiasa.

Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza, ulikuwa na zaidi ya wapiga kura milioni 2.3 mwaka 2020. Mkoa huo mara zote umekuwa kiini cha ushindani mkali wa kisiasa kutokana na historia yake ya upinzani na pia nguvu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kijadi.

Kuhusu Mbeya, ulikuwa na zaidi ya wapigakura milioni 1.8. mkoa huo wa Mbeya mara nyingi hujulikana kama ngome yenye msimamo mkali, vyama vya upinzani viliwahi kupata mafanikio makubwa, lakini tayari utafiti unaonyesha CCM imewekeza nguvu zaidi kwa miaka ya hivi karibuni ikilenga kuimarisha mizizi yake.

Dodoma, ndiyo makao makuu ya nchi. Na ni mkoa uliokuwa na zaidi ya wapigakura milioni 1.7 mwaka 2020, uzito wa kipekee kwa sababu ya siasa za kitaifa na kuwapo kwa taasisi kuu za dola.

Kagera na Tabora ni mikoa iliyokuwa na zaidi ya wapigakura milioni 1.5 kila mmoja, yenye historia ya ushawishi mkubwa, hasa kutokana na muundo wake wa kijamii na kiuchumi.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Matrona Kabyemela anasema mikoa hiyo ni msingi mzuri kwa wagombea kuweka mikakati ya kuwafikia wapigakura kulingana na maeneo wanayokubalika na wingi wa wapigakura.

“Kama mgombea alipanga kufanya kampeni katika eneo moja kwa muda mrefu, sasa kupitia takwimu hizo anajua eneo hilo lina wapiga kura wangapi, anakubalika hapo au atumie muda mfupi eneo hilo aende jimbo lenye wapigakura wachache na anakubalika,” anasema.

Dk Kabyemela anasema wakati wa kampeni za uchaguzi vyama hutafuta namba za wapigakura kwa ajili ya kushinda uchaguzi mkuu.

“Takwimu hizi ni nzuri wakati wa kampeni, vyama vitajua namna gani zigawanye rasilimali fedha kulingana na wingi wa watu ambao inaamini itawawezesha kushinda uchaguzi,” anasema.

Katika mkoa wa Dar es Salaam, majimbo yenye wapigakura wengi ni Temeke wapiga kura 560,788, Segerea 545,797, Kawe 532,173, Ubungo 424,693, Kibamba 407,629, Kinondoni 366,234, Arusha 435,119, kwa upande wa Mwanza Jimbo la Nyamagana 436,774, Ilemela 367,205 na Morogoro mjini 366,078.

Kwa upande wake Mchambuzi wa masuala ya siasa Mwalimu Samson Sombi amesema idadi ya wapiga kura kwenye jimbo inaweza kuwa kubwa lakini kampeni ndio ikaamua idadi ya watakaopiga kura.

“Lazima wagombea wahakikishe wanapokwenda kwenye majimbo hayo wananadi sera zinazoeleweka, wasiongee mambo yasiyotekelezeka, wapiga kura sasa wanaelewa, watu wanajitokeza kwenye kampeni kwa kuvutiwa na wagombea na sera,” amesema.

Amesema endapo kampeni zitakuwa na fujo na wagombea kutokuwa na mvuto licha ya kuwa majimbo hayo kuwa na wapiga kura wengi, watakaojitokeza kupigakura watakuwa wachache.

Hayo yote yanakuja, wakati ambao zimebaki siku tisa kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu kuzinduliwa.

Hata hivyo, vyama mbalimbali vya siasa, vimeonekana vikipita huku na kule kuomba udhamini kwa wagombea wake wa urais.

Chama cha ACT Wazalendo kimeanza ukusanyaji wa wadhamini katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu na mingine ya Kanda ya Ziwa inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya wapigakura.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 uliokuwa na wagombea 15 wa nafasi za urais wa Tanzania, mgombea wa Chama cha Mapinduzi, hayati Rais John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 12.5 akifuatiwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu aliyepata kura milioni 1.9.

Kwa wakati huo, idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura mwaka 2020 ni milioni 29.7 tofauti na sasa ambapo wapiga kura milioni 37.65 wamejiandikisha ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.55.

Mchambuzi wa siasa, Majjid Salim anasema kwa chama makini, kitawekeza nguvu zaidi kwenye mikoa yenye idadi kubwa ya wapigakura.

Uwekezaji huo, anasema unaanzia kwenye kutoa elimu ya mpigakura na kufanya shughuli za mapema kabla ya kampeni ili kuhakikisha chama husika kinajulikana.

Baada ya kujulikana, anaeleza chama husika kinapaswa kujenga ushawishi kwa wapigakura, sio wanachama wake pekee, bali watu wote waliopo katika mkoa husika.

Hilo, anasema linafanywa kwa kujenga hoja na kueneza sera za chama husika, huku wakati wa kampeni ukisubiriwa kwa ajili ya kufukia mashimo na kuhitimisha.

Kwa wanasiasa ambao hawakuwekeza kwenye mikoa hiyo, ameeleza wanapaswa kutoa kipaumbele cha ziara wakati wa kampeni.

“Yaani wahakikishe wanatumia siku nyingi kufanya kampeni kwenye maeneo hayo, kuliko mikoa mingine ambayo wanajua kabisa ina kura chache,” anasema.

Kufanya hivyo, anasema kunakisaidia hata chama chenye rasilimali chache kuzitumia katika maeneo machache lakini yenye mtaji mikubwa wa wapigakura.

Sambamba na hilo, anaeleza wingi wa wapigakura katika maeneo hayo unatokana na idadi kubwa ya watu katika eneo husika, hasa ukizingatia ni mikoa ya kibiashara.

“Mkoa kama Dar es Salaam, watu hawapo tu kwa ajili ya makazi, bali wanafuata biashara, wanaunganishwa na wingi wa fursa, ndiyo maana wapo wengi na hivyo wapigakura watakuwa wengi,” anasema.

Salim anasisitiza wingi wa wapigakura ni kipimo cha ushindi kwa mgombea husika, lakini kuupata inategemea umezichanga vipi karata zako.

Anasema hata kihistoria ushindi wa wagombea wengi wa urais nchini, ulibebwa na kura za mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa mingine mikubwa ambayo aghalabu CCM huwezeka nguvu.