Maema aiwahi Simba Misri | Mwanaspoti

KIUNGO mpya wa Simba, Neo Maema ataungana na kikosi cha timu hiyo kambini jijini Cairo nchini Misri leo tayari kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Maema alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ kilichokuwa kinashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024.

Hata hivyo, juzi Bafana Bafana ilishindwa kuingia hatua ya robo fainali baada ya kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Uganda jambo lililoifanya itupwe nje ya mashindano hayo yatakayofikia tamati Agosti 30, 2025.

Chanzo cha uhakika kutoka katika kambi ya Simba iliyopo Misri kimethibitisha kuwa leo kiungo huyo ataungana na wenzake kambini.

“Maema anaungana na kikosi leo,” kimefichua chanzo hicho.

Maema katika fainali za CHAN ndio alikuwa nahodha wa Afrika Kusini na amemaliza mashindano hayo akiwa amefunga bao moja katika mechi nne alizocheza.

Katika hatua nyingine, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa jezi mpya za timu hiyo zitazinduliwa Jumatano ijayo.

“Jezi za Simba msimu huu tutaenda kuzizindua kwa namna tofauti kidogo. Jezi za Simba zitazinduliwa 27.08.2025. Jezi zitazinduliwa kuanzia saa 1:00 usiku katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki.

“Kwa kipekee kabisa kwenye kuongezea thamani tukio letu, tutakuwa na mchezaji wa zamani wa soka barani Afrika ambaye anafahamika dunia nzima. Tutamtambulisha siku chache zijazo.

“Yeyote ambaye anataka kushiriki tukio hilo, atalipa Sh250,000. Mara baada ya uzinduzi huo, jezi za Simba SC zitaanza kuuzwa katika maduka yote ambayo yameweka oda za awali,” amesema Ally.