Mfuko wa mikopo wa Serikali waja na mkakati utekezaji wa Dira 2050

Arusha. Katika hatua ya kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Taasisi ya Self Microfinance Fund (Self Fund), imetaja mipango ya kukuza sekta ya uchumi nchini ambayo katika dira hiyo huduma za kifedha zinatajwa kama moja ya kichocheo muhimu cha mageuzi ya kiuchumi Tanzania.

Dira hiyo ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025, inalenga kuijenga Tanzania ya baadaye inayotegemea ubunifu wa kidijitali kwa ajili ya tija, ustawi wa wananchi na ujumuishaji wa kifedha kwa wote.

Taasisi hiyo iliyopo chini ya Wizara ya Fedha imeainisha nia yake ya kusaidia wananchi wa kipato cha chini ili kuwapa fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na hivyo kujiongezea kipato.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 20, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Paul Sangawe, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, kuhusu mipango ya kuimarisha huduma katika kipindi cha miaka mitano 2025 hadi 2030.

Amesema kwa kuzingatia Dira hiyo na kwa fursa zilizopo wanajipanga kuboresha utekelezaji wa majukumu yao na hivyo kuwa sehemu ya utekelezaji wa Dira hiyo pamoja na mafanikio mengine kwa Taifa.
“Kwa kipindi cha mwaka 2025/30 tunatoa kipaumbele katika maeneo makubwa ikiwemo kuwa na mpango mkakati wa muda mrefu na unaozingatia maeneo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, na yatakayoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Muda mrefu (LTPP) na kimataifa.”

“Kuongeza mtaji wa mfuko ili kupanua wigo wa kuhudumia wateja, kuimarisha ushirikiano na wadau wengine hususan taasisi nyingine za kifedha na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,”amesema.

Mwenyekiti huyo amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2021/25 mfuko huo umeongeza mtaji kutoka Sh58.47 bilioni hadi kufikia Sh59 bilioni mwaka 2024.

Nyingine ni kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh196.9 bilioni, kuzalisha ajira kwa wanufaika 183,381 katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuimarisha taasisi ndogo za fedha 549 kwa kuwapatia mikopo na mafunzo ili kuziwezesha kutoa huduma bora.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Santieli Yona amesema wamelenga kupanua wigo wa huduma zao na kufikia wananchi wengi ili wanufaike na mikopo na kuepukana na mikopo umiza.
Amesema tangu 2015 hadi sasa wameshatoa mikopo ya zaidi ya Sh397 bilioni   kwa makundi mbalimbali ikiwemo wajasiriamali, kilimo na nishati safi ya kupikia.

Sambamba na hilo, pia  wanaendelea kutoa elimu kwa wanufaika ili kuondoa changamoto za ukosefu wa uelewa na urejeshaji mikopo.
“Tunatoa mikopo hii nafuu kwa makundi mbalimbali kwa ajili ya kukuza biashara zao na shughuli nyingine za kujipatia kipato wakiwemo wanawake na vijana ambapo wengine wameanzisha biashara na kuongeza kipato,”amesema.