Mkenya aipa ushindi Stars kwa Morocco

KOCHA Msaidizi wa Singida Black Stars, Mkenya David Ouma ameipa nafasi kubwa Taifa Stars kushinda dhidi ya Morocco katika robo fainali ya michuano ya CHAN.

Taifa Stars imetinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo 2009, baada ya mara mbili zilizopita 2009 na 2020 kushindwa kuvuka hatua ya makundi.

Safari hii Taifa Stars imekuwa moto baada ya kumaliza kinara wa kundi B ikishinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Burkina Faso (2-0), Mauritania (1-0), Madagascar (2-1) na sare dhidi ya Afrika ya Kati, jambo liloiweka kileleni kwa alama 10.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema kuelekea mchezo huo ambao utapigwa Ijumaa hii, Agosti 22 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam, anaipa nafasi kubwa Tanzania kutokana na ubora wa kikosi chake.

Alisema wachezaji wa Taifa Stars wamekuwa na ukomavu na ujasiri wa kimaifa kutokana na mazingira magumu ya ushindani wa Ligi Kuu Bara, ambayo sasa imejaa nyota kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na Amerika Kusini.

“Ligi ya Tanzania imeimarika sana ndio maana hata wachezaji wa Stars wanaweza kucheza na timu yoyote ile bila presha na wakashinda, hivyo naamini hata dhidi ya Morocco watashinda,” alisema Ouma.

Kocha huyo alisema umoja wa timu, kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji, umeifanya Taifa Stars kuwa tishio na kupata matokeo bora dhidi ya wapinzani.

Ouma aliongeza kuwa wachezaji sasa wana uzoefu na ujasiri wa kutafuta suluhisho tofauti kila wanapokutana na changamoto, hali ambayo imeifanya Taifa Stars kuwa tishio kwa timu kubwa kama Morocco.

Pia alilipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa maandalizi bora ya michuano hiyo kupitia mashindano ya Cosafa, kambi ya Misri na mashindano ya Cecafa Arusha akisema yote yamechangia mafanikio haya.

Kwa mujibu wa Ouma, safari ya Taifa Stars kuelekea kubeba ubingwa inaanza kwa kuiondoa Morocco, akisisitiza kila mchezaji anapaswa kucheza kwa bidii na nidhamu ili kufanikisha malengo ya taifa.

Mabingwa mara mbili wa michuano hiyo mwaka 2018 na 2020, timu ya taifa ya Morocco ilimaliza nafasi ya pili kundi A kwa alama tisa baada ya mechi nne, huku vinara wakiwa ni Kenya kwa alama 10.