Mara nyingi nilipokwenda hospitali kutibiwa, niligundua kuwa madaktari walikuwa wakikariri tiba. Kabla sijajieleza, daktari aliyatazama macho yangu mekundu na kuandika tiba ya malaria.
Hata katika eneo lililowekewa karantini kutokana na ugonjwa kipindupindu, macho na akili za matabibu huangukia kwenye mlipuko huo. Ikitokea mtu amekula kiporo akavurugwa na tumbo, haraka sana ataingizwa kundini.
Haya ndiyo matatizo ya mazoea. Wakati huu tunaposhuhudia homa ya uchaguzi ikipamba moto, kila tukio linachukuliwa kuwa cheche za Uchaguzi Mkuu.
Kwa vile imezoeleka kuwa wakati kama huu watu wanafanyiana figisu, basi hata magari yakigongana yatahusishwa na wagombea au vyama. Uchaguzi umekuwa kama jinamizi linalotishia usingizi wa mahasimu wa siasa na wananchi kwa ujumla.
Mbali na uchaguzi, maisha mengine yanaendelea kama kawaida. Vibaka wanapora, walozi wanaroga, waumini wanaabudu na jua linakucha na kuchwa. Waswahili walimwambia jogoo “uwike usiwike kutakucha!”
Yaani hawezi kuzuia mapambazuko kwa kugoma kuwika. Hivyo uswahilini matukio mengine yanaendelea kutokea pamoja na kwamba tungali tunasubiri Uchaguzi Mkuu.
Hivi karibuni wakazi wa Geita wamevamia msitu wa hifadhi na kuuchoma moto pamoja na kuharibu miundombinu ya hifadhi hiyo. Hili halihusiani na uchaguzi, ila watu wenye hasira kali wamefanya tukio pengine kupunguza hasira, kujifariji, kulipa kisasi au kutuma ujumbe kwa yeyote anayehusika na mateso yao.
Wameonesha kudhamiria jambo hilo kwani hawakuwa na hofu ya kuficha utambulisho wa majina na sura wakati wakitoa taarifa.
Polisi wametangaza kuwakamata baadhi ya walioshukiwa kufanya tukio. Wakasema watashughulika nao kwa makosa ya kujichukulia sheria mikononi. Bila shaka uchunguzi wa kina utafanyika ili watakaodhihirika kufanya makosa watiwe hatiani. Na bila shaka suluhisho halitachukua muda mrefu kutokana na mazingira ya tukio, na kwa jinsi sheria ya kesi yenyewe ilivyo wazi.
Mimi nina mengi ya kusema kutokana na tukio hilo. Mimi nachukulia kuishi jirani na msitu au hifadhi kuwa fursa.
Pamoja na kuambulia baraka za hewa safi na mvua, majirani hupata vyanzo vya majisafi pamoja na kuni kwa matumizi yasiyowezekana kwa nishati safi.
Si rahisi kupika mbege kwa kutumia gesi, hivyo mabaki ya miti huweza kutumika kwenye shughuli kama hizo.
Lakini ili kuepuka uharibifu ndani ya hifadhi, Wakala wa Misitu huweka wataalamu na walinzi, pamoja na kanuni za matumizi ya maliasili ili kuhifadhi.
Wasimamizi hao huelekezwa kushirikiana na wananchi, pamoja na kuwafundisha yale yasiyofahamika na umma kuhusu afya ya msitu. Lakini pia wasimamizi hupokea uzoefu kulingana na historia ya eneo hilo kutoka kwa wenyeji.
Sasa kumekuwa na kutokuelewana kati ya wadau hao.
Wananchi wanadai kuwa Wakala wa Misitu umewaletea waangalizi wasio waadilifu, na wanaokiuka sheria ya haki za binadamu. Wamedaiwa kukamata mifugo na kuwapiga wachungaji faini wasizoweza kuzilipa.
Uongozi wa Kijiji umekiri kushirikishwa kwenye mashauri, ambapo wanakijiji walitozwa faini ya mamilioni ya fedha yaliyokuwa nje ya uwezo wao.
Mbaya zaidi, walinzi wamelalamikiwa kwa kuwavizia na kuwakosea kinamama na wasichana wanaoingia msituni.
Imedaiwa matukio haya hufanyika katika nyakati za alfajiri na usiku pale wahanga wanapowahi au kuchelewa msituni.
Wakati mwingine hata mchana kweupe wanapoingia pasipo mashuhuda, walinzi huwadhalilisha kijinsia pamoja na kuwabaka bila kuthamini utu wao.
Lakini mimi ninapoliangalia suala hili kwa jicho la tatu, naona shaka pale wananchi wanapofanya jambo zito kama hilo na kujitokeza hadharani kusimulia.
Angelikuwa mtu mmoja ndiye aliyejitokeza ningedhani ni mtu aliyevurugukiwa na akili. Mtu mwenye akili timamu angechelea kurukiwa na vyombo vya dola.
Lakini wanaojitokeza ni kikundi au umoja wa wanakijiji unaozidi watu kumi. Kwa sababu watenda na watendwa wote ni wanadamu, jambo hilo linaweza kuwa limefanyika au halijafanyika.
Ni jukumu la mamlaka na vyombo shirikishi vya umma kufanya uchunguzi wa kina. Uchunguzi usimamiwe na vyombo vya dola lakini pia asasi za kiraia ili kupata mzani halisi. Iwapo wataachiwa Polisi pekee, kuna hatari ya upande mmoja kukosa haki maana adhabu imeshaandaliwa. Nasema hivi nikiyatazama maisha yetu ya kila siku huku mtaani. Kasi watu kutoana roho iko juu na inazidi kupanda. Kisa kinachoongoza kutajwa ni “wivu wa mapenzi.”
Mapenzi yanajulikana kuwa ni tiba ya uhakika, lakini kama zilivyo tiba zingine, hugeuka sumu kali inapotumiwa vinginevyo. Baadhi ya wanazuoni hukiri kuwa ibilisi ameweka makazi kwenye sehemu mbili tu; penye riziki na penye mapenzi.
Sasa chukulia kuwa matendo hayo yametendeka ukweli. Tufanye vijana watunzaji wa hifadhi wamewabaka wake za watu pamoja na mabinti zao.
Hatuna ushahidi, ila ninachotaka ni kuwaza tu kwamba tukio hilo limetokea.
Hakika tukivaa viatu vya wananchi walioporwa haki ya ndoa zao (tena kwa mabavu) tunaweza kufikiria makubwa. Unaweza ukasema angeweza kufanya makubwa zaidi ya kuchoma msitu.
Ila nawaasa Wakala wa Misitu wachague wafanyakazi wenye kiu ya kujifunza tamaduni mbalimbali. Hata hivyo naomba Mungu atuepushe na laana hizo.