Nishati safi yapunguza gharama Shule ya Nyamunga 

Mara.Shule ya Sekondari Nyamunga wilayani Rorya, Mkoa wa Mara imefanikiwa kupunguza gharama za matumizi ya nishati ya kupikia kwa asilimia 38 kila mwezi, kutoka Sh1.6 milioni hadi Sh1 milioni baada ya kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Mafanikio hayo yametajwa kuwa kielelezo cha namna jamii na taasisi zinavyoweza kupunguza gharama na kulinda mazingira iwapo zitaacha utegemezi wa kuni au mkaa.

Akitoa taarifa mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa leo Agosti 19, 2025, Mkuu wa Shule ya Nyamunga, Patrick Wadugu amesema  Sh11 milioni zilitumika kugharamia mradi wa nishati safi katika shule hiyo.

“Tulisimika na kufunga majiko matatu ya gesi. Katika miezi miwili pekee tuliyoanza kutumia matokeo yake ni makubwa, tumepunguza gharama za uendeshaji na tunawaandalia wanafunzi chakula kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Wadugu amesema mradi huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza matumizi ya nishati isiyo salama, lengo ni kufikisha asilimia 80 ya matumizi ya nishatisafi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Akizindua rasmi mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi amewataka wananchi kuanza kutumia nishati safi.

Amesema hatua hiyo inalinda afya, inapunguza gharama na inalinda mazingira.

“Uharibifu wa mazingira unachochewa na matumizi ya kuni na mkaa. Rais wetu amesisitiza mara nyingi kwamba, matumizi ya nishati safi ni kinga kubwa kwa mazingira na afya zetu,” amesema.

Rhobi Magesa, mmoja wa wapishi amesema awali walikuwa wanakumbana na moshi na kutumia muda mrefu kuandaa chakula, lakini sasa kazi zao zimekuwa rahisi.

“Zamani tulikuwa tunatumia muda mrefu sana kuandaa vyakula lakini pia moshi ulikuwa unatutesa sana, kuna wakati tulikuwa tunatumia kuni mbichi kwa hiyo tulikuwa tunapata shida sana kupika,”amesema Rhobi Magesa.

Naye Mkazi wa Kijiji cha Nyamunga, Boaz Mane amesema gesi ni suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa kuni.

“Miti imekatwa kupita kiasi na hata hali ya hewa imebadilika. Sasa hivi gesi ndiyo mkombozi wa familia na hasa wanawake wanaojihusisha na mapishi,” amesema.