KOCHA wa Yanga, Romain Folz bado anaendelea kukijenga kikosi cha timu hiyo mdogomdogo na jana asubuhi kilikuwa pale Fukwe za Coco, jijini Dar es Salaam.
Yanga ilikuwa hapo kwa takribani saa mbili ikiwa na mastaa wake wote wakiwemo viungo Moussa Bala Conte, Pacome Zouzoua na Ecua Celestine, lengo likiwa ni kufanya mazoezi ya ufukweni kuongeza utimamu wa mwili.
Zoezi hilo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Agosti 15, mwaka huu kucheza mechi ya kirafiki Rwanda dhidi ya Rayon Sports na kushinda kwa mabao 3-1, lakini utimamu wa wachezaji kimwili ulionekana kuwa chini huku kocha wa mazoezi ya viungo, Tshephang Mokaila hivi karibuni kusema anaona bado hawajafika hata asilimia 40 ya wanapotaka kufika.
Kwenye programu hiyo, mchora ramani alikuwa Mokaila na aliongoza kila kitu kwenye kila aina ya mazoezi.
Mokaila alikuwa gumzo kwenye mazoezi hayo kama kawaida yake akitangulia kufanya mwenyewe kwa utimamu ‘demo’ kisha wachezaji wake wanafuata.
Hata hivyo, wakati Mokaila akisimamia, Folz na wasaidizi wake walikuwa wakifuatilia kila hatua wakihakikisha hakuna mchezaji anayefanya tofauti au kutegea.
Kila mchezaji alikuwa akijituma kwenye mazoezi hayo huku wakionyesha kuteseka kutokana na ugumu wa kukimbia kwenye mchanga.
Baada ya mazoezi hayo ya mbio tofauti, kikosi hicho kiliuchezea mpira kidogo kwa timu mbili tofauti hapohapo ufukweni, kisha kufunga ratiba hiyo.
Kikosi hicho kimeendelea kujiimarisha kwenye utimamu wa mwili kikijipanga na msimu mpya wa 2025-2026 ambao Folz atakuwa na kibarua cha kuiongoza Yanga kutetea mataji iliyoyachukua msimu uliopita ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Muungano.
Baada ya jana, leo Jumatano kikosi hicho kitarudi uwanjani kuendelea na mazoezi mengine, yanayoendelea Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar.