MZIKI wa Simba unaosukwa huko Misri, umeibua jambo jipya kutokana na nyota saba kuonekana kufumua kikosi cha kwanza ambacho awali kilikuwa kinampa jeuri Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Fadlu ambaye anaingia msimu wa pili kuinoa Simba, alikuwa na wakati mzuri 2024-2025 kwani licha ya kutotwaa taji lolote, lakini kuna mabadiliko makubwa yametokea hasa kwenye ushindani katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Kabla ya ujio wa Fadlu, Simba ilikuwa imecheza robo fainali sita za michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuanzia 2018 na kushindwa kusonga mbele, lakini Msauzi huyo akaifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wake wa kwanza 2024-2025 na kukosa ubingwa mbele ya RS Berkane kwa matokeo ya jumla 3-1, kufuatia ugenini kufungwa 2-0 na nyumbani kutoka 1-1.
Kufikia hapo, ndipo mabosi wa Msimbazi wakaona kuna kitu kizuri kinakuja siku za usoni.
Mbali na hilo, Simba iliyoukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo ukibebwa na watani zao wa jadi, Yanga, ilishuhudiwa msimu wa 2023-2024 ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Yanga na Azam iliyomaliza ya pili. Fadlu akaipandisha Simba nafasi moja na kumaliza ya pili msimu uliopita nyuma ya mabingwa Yanga.
Kupiga hatua kadhaa kwa Simba, kumewafanya mabosi wa klabu hiyo kumpa mahitaji yote Fadlu katika usajili ndiyo maana hadi sasa kuna majembe ya maana yameshuka Msimbazi yakiendelea kujifua huko Misri huku mengine yakiwa njiani kuungana na wenzao kutoka kwenye michuano ya CHAN.
Hadi kufikia sasa, Simba imetambulisha rasmi kusajili wachezaji wapya wanane ambao ni Anthony Mligo, Naby Camara, Rushne De Reuck, Alassane Kante, Semfuko Charles, Morris Abraham, Mohammed Bajaber na Jonathan Sowah, huku Neo Maema na Yakoub Suleiman duru zikibainisha muda wowote nao watatambulishwa kwani kila kitu kipo kama walivyopanga.
Kabla ya ujio wa nyota hao wapya, kikosi cha kwanza cha Simba msimu uliopita ambacho Fadlu alikuwa akionekana kinampa jueri kubwa kilikuwa kinaundwa na Mousa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Chamou Karaboue, Che Malone Fondoh, Yusuph Kagoma, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua na Elie Mpanzu.
Katika kikosi hicho, awali Chamou alikuwa akisubiri mbele ya Abdulrazack Hamza, lakini baadaye akapindua meza kufuatia Hamza kupata majeraha ya mara kwa mara. Pia Ateba akawa anapishana na Steven Mukwala hali iliyofanya kumaliza msimu kila mmoja akifunga mabao 13 kwenye ligi. Mwingine aliyepenya dakika za mwisho alikuwa Joshua Mutale, huku wengine wakibaki kushikilia utawala wao kikosi cha kwanza.
Kuondoka kwa Tshabalala aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Che Malone na Ngoma, huku Ateba naye akitajwa kuaga kambini, kumemfanya Fadlu kushusha mashine zingine za maana ambazo moja kwa moja zinakwenda kuingia kikosi cha kwanza kuchukua nafasi zao.
Nyota hao ni Rushne De Reuck anayecheza beki wa kati nafasi ya Che Malone, Naby Camara mwenye uwezo wa kucheza beki wa kushoto na kiungo akitazamiwa kuwa mbadala wa Tshabalala, huku Alassane Kante akienda kuvaa viatu vya Ngoma. Kule mbele kuna Jonathan Sowah, mshambuliaji aliyetokea Singida Black Stars ambaye msimu uliopita alitua dirisha dogo na kumaliza ligi akifunga mabao 13, matatu nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua.
Ukiweka kando wachezaji hao wanne ambao wanaingia moja kwa moja kikosini kufuatia waliokuwepo kuondoka, kuna eneo linakwenda kutikiswa kwani majembe mapya mawili, Bajaber na Maema yana kitu mguuni, hivyo kuna kazi ya waliopo kukaza buti kuendelea kushikilia nafasi zao.
Wachezaji ambao wanakwenda kutikiswa ni kinara wa mabao Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Jean Charles Ahoua na Kibu Denis.
Bajaber ana uwezo wa kucheza winga zote mbili ambazo ni kushoto na kulia, sambamba na mshambuliaji wa pili kwa maana ya namba kumi. Katika nafasi hizo mbili, msimu uliopita ndani ya Simba ulikuwa ni utawala wa Kibu (winga) na Ahoua (mshambuliaji wa pili).
Maema naye hayupo mbali na Bajaber kwani pia anacheza eneo la kiungo mshambuliaji, pia winga ya kulia na kushoto.
Kwa ujumla, wachezaji wapya ambao wametua Simba hadi sasa, unaweza kusema watano wana uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza kutokana na ubora wao kulinganisha na waliowakuta, huku wawili wakiweka hatiani nafasi za watu na kufanya jumla yao kuwa saba.
Ukiangalia maeneo mengine yaliyopo salama ni kipa akitarajiwa kuendelea kusimama Moussa Camara licha ya kuwepo taarifa za ujio wa Yakoub Suleiman. Kapombe bado ana nafasi ya kusalia kucheza beki wa kulia akimsubirisha David Kameta ‘Duchu’. Pale kati, Chamou Karaboue ana nafasi yake kama ilivyo kwa Yusuph Kagoma eneo la kiungo cha ukabaji na Elie Mpanzu eneo la winga mojawapo.
Akizungumzia maendeleo ya kikosi chake, Fadlu alisema: “Katika maandalizi ya msimu kunahitajika umakini wa hali ya juu kwa maana ya kuandaa kikosi imara. Ndiyo maana tunapata muda mwingi wa kuwaangalia (wachezaji) na kufanya nao mazoezi yatakayoleta ushindani katika michuano mbalimbali itakayokuwa mbele yetu.
“Mazoezi yananipa matumaini ya mbele kutatengenezwa kitu kikubwa na kizuri ambacho kitazaa matunda baada ya kuanza majukumu yetu ya msimu ujao.”