Unguja. Katika kutatua changamoto za watu wenye ulemavu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetaja hatua inazochukua ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wao katika ngazi za uamuzi kutoka asilimia mbili za sasa hadi tano ifikapo mwaka 2030.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Agosti 20, 2025 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman wakati akizindua programu ya kuinua haki za watu wenye ulemavu ya CADiR (Collective Action for Disability Rights), ambao ni mpango wa miaka mitano wa kukuza na kuimarisha haki za watu hao Tanzania bara na Zanzibar.
Othman, amesema licha ya juhudi zinazotekelezwa na Serikali, kwa kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu nchini, bado mahitaji yao ni mengi, hivyo mradi huo utaongeza uwezo wa kulifikia kundi hilo na kuhamasisha upatikanaji wa haki, fursa kwa ajili ya maendeleo yao.
“Serikali imepanga kuwatambua wao na mahitaji yao kwa kuimarisha mifumo ya utambuzi wa awali wa ulemavu na kuchukua hatua stahiki katika wakati muafaka,” amesema.
Watoto wenye ulemavu wakiimba wakati wa kuzindua mradi wa kuimarisha haki za watu wenye ulamavu iliyofayika Unguja Zanzibar
Ametaja hatua zingine zinazochukuliwa ni pamoja na kuweka taasisi za watu wenye ulemavu chini ya viongozi wakuu wa nchi, kutunga sera na sheria, kuanzishwa chombo cha kusimamia na kuratibu masuala ya ulemavu na kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo.
Serikali kuimarisha huduma za kijamii, kuanzishwa kwa Taasisi ya Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea) kupitia programu ya 4.4.2, pia mwaka 2025/30 Serikali imepanga kuimarisha ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu na kuanza ujenzi wa kituo cha marekebisho na ahueni kwa walemavu.
Hivyo, Othman ametoa wito kwa kila mmoja achukulie suala la haki na fursa kuwa jambo la wajibu nchini, linalohitaji ushirikiano ili kujenga jamii bora yenye ustawi.
Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Watu Wenye Ulemavu Norway (NAD), Abdulla Amair amesema lengo la mradi huo ni kuongeza upatikanaji wa haki za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi za chini hadi juu.
Pia, amesema shule 110 zinatarajiwa kufikiwa kwa kutengeneza moduli za kuwafanya watu hao watoe huduma na wachukuliwe kama watoa huduma na sio wahitaji huduma pekee jambo ambalo litawasaidia kufanya kazi katika taasisi za Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (Shijiwaza), Mwadawa Khamis Mohamed ameishukuru Serikali kwa kutoa kipaumbele kwao kushiriki katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuzijengea uwezo jumuiya hizo.
Ametoa wito kwa watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa zinazotolewa kwa kuhakikisha hawabaki nyuma.
Naye Katibu wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe amesema mradi huo una lengo la kufikia jamii jumuishi na kujenga ushiriki wa watu wenye ulemavu katika miradi ya maendeleo kwani, wamekuwa wakibaki nyuma katika jitihada hizo kutokana na mazingira magumu na ukosefu wa vifaa saidizi.
Mwenyekiti wa Shijawata, Tungi Mwanjara amesema wapo kwa ajili ya upatikanaji wa haki za walemavu na kuzingatiwa kwa namna mbalimbali bila kuachwa nyuma.
Waziri wa Afya Zanzibar, Ahmed Mazrui amesema wizara hiyo inahakikisha inashiriki katika mnyororo wa watu wenye ulemavu tangu mimba inapotungwa hadi mtoto kuzaliwa ili kuepusha watoto kuzaliwa na ulemavu unaozuilika.
“Kuna ulemavu unaozuilika, kwa hiyo wizara tumejipanga kuhakikisha mjamzito anaanza kliniki anapata huduma zote tangu mimba hadi mtoto anapozaliwa,” amesema Mazrui.
Mradi huo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2029 una thamani ya Sh20 bilioni ambao utasaidia katika elimu jumuishi, afya na uwezeshaji kiuchumi kwa watu wenye ulemavu.