Takwimu zitumike kufanya maamuzi ya kimkakati ili kilimo kiwe na tija.

Arusha. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema ipo haja ya kuweka mipango inayotekelezeka ya kutumia takwimu za kilimo na masoko zilizokusanywa kufanya maamuzi ya kimkakati ili kufikia malengo yanayokusudiwa.

Hayo ameyasema leo Jumatano, Agosti 20, 2025 wakati akifungua mkutano wa wadau wa kilimo kutoka nchi wanachama wa Soko la Pamoja Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuhusu mifumo ya taarifa za masoko ya mazao ya mbogamboga na matunda.

Meneja Mkuu wa Masoko wa taasisi ya Taha inayojihusisha na mazao mbogamboga na matunda,Anthony Chamanga akizungumza katika mkutano wa kanda za Comesa na EAC jijini Arusha leo.Picha na Filbert Rweyemamu



Amesema mkutano huo utawezesha kutanua masoko ya mazao ya mbogamboga na matunda kupitia kanda hizo mbili ikiwa ni pamoja na kuweka mipango madhubuti ya pamoja inayolenga kuongeza uzalishaji kutoka kwa wakulima.
“Kimsingi takwimu za shughuli za kilimo kwenye nchi zetu zimekua zikikusanywa na wataalamu wetu, changamoto kubwa imekua kutumia takwimu hizo kufanya maamuzi ya kimkakati yanayoweza kuleta tija katika mnyororo mzima wa kilimo,”amesema Mweli

Mweli amesema mifumo ya taarifa za nchi za EAC na Comesa ambazo zina jumla ya nchi 29 zinapaswa kusomana ili kuwezesha wadau wa kilimo kupata taarifa sahihi zitakazotumiwa kupanga mipango inayotekelezeka ikiwa ni pamoja na kupata masoko ya mazao ya mbogamboga na matunda ndani na nje ya kanda hizo.

Katibu Mkuu huyo amesema kupitia takwimu sahihi Tanzania imefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda ndani ya kipindi cha miaka minne kutoka tani milioni mbili hadi tani milioni saba.

“Hizi ni takwimu tulizonazo ila naamini tukiimarisha uwezo wa kukusanya takwimu zitatuonesha wakulima wa mazao hayo ni wengi zaidi na tutaweza kujua wanatumia mbegu za aina gani, aina na kiwango cha mbolea na iwapo maofisa ugani wanawafikia pia anauza wapi baada ya kuvuna. Na hizi taarifa ziwekwe kwenye mfumo wa pamoja.
Ameongeza kuwa maazimio ya mkutano huo yatasambazwa katika nchi wanachama kwa ajili ya utekelezaji kulingana na mikakati ya kila nchi na Tanzania ina mpango wa 2030 unaolenga kukuza ukuaji wa kilimo kwa mwaka kufikia asilimia 10, kutoka asilimia nne iliyopo sasa .


Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Maendeleo wa Taasisi ya Taha, Anthony Chamanga amesema mkutano huo ni muhimu kwani unawezesha wataalamu wa kilimo kutoka nchi wanachama kubadilishana uzoefu wa ukusanyaji wa taarifa, takwimu na usambazaji wake.

“Taarifa zinatusaidia kufahamu fursa zinazopatikana kwenye kanda za Afrika,nchi zote tunazalisha mazao ya mbogamboga na matunda.

Chamanga ameongeza kuwa kupitia taasisi ya Taha wanao mfumo wa mfano wa kukusanya taarifa za kilimo zikiwemo takwimu za masoko, uzalishaji na wanunuzi wa mazao hayo nchini na nje ya nchi zinazotumiwa na wadau kwenye kufanya maamuzi.

Amesema sekta ya mazao ya mbogamboga na matunda inakua kwa kasi kubwa hivyo ni muhimu kupanua wigo wa masoko kwenye nchi nyingine za Afrika.

“Kwa sasa Tanzania inauza ndizi zisizopungua tani 2,000 kwa mwaka nchini Zambia hatua inayowaongezea wakulima mapato.”

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Asasi ya Uendelezaji wa Biashara ya mazao katika nchi za Soko la Pamoja Mashariki na Kusini mwa Afrika (ACTESA), Dk John Mukuka amesema mifumo ya takwimu itawasaidia wadau walio katika mnyororo wa sekta ya kilimo kuzalisha wakiwa na taarifa sahihi.