TRC kumwaga ajira 2,460 SGR

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania linatarajia kuajiri wafanyakazi 2,460 katika mradi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa vipande viwili vya kutoka Dar es Salaam mpaka Makutopora.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Agosti 20, 2025 katika kurasa za mitandao ya kijamii ya TRC, imeeleza kuwa ajira hizo ni mbali na zaidi ya ajira 115,000 ambazo tayari zinatokana na mkandarasi katika kipande cha kwanza mpaka cha sita.

Katika ajira hizo 2,460 utekelezaji wake ni wa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 zaidi ya watumishi 500 wameshaajiriwa.

Imeeleza kuwa mwaka huu wa fedha 2025/2026 matarajio ni kuajiri watumishi 272 na TRC itaendelea kuajiri mpaka kufikia watumishi 2,460.

“Wakati utekelezaji wa utoaji ajira rasmi za Shirika ukiendelea, jumla ya ajira 115,000 kutoka kwa mkandarasi zimeshawanufaisha Watanzania 115,000 zikiwemo za vijana wa elimu ya darasa la saba na viwango vingine vya elimu katika fani mbalimbali.”

“Mchanganuo wa ajira hizo 115,000 kutoka kwa mkandarasi ni kwamba ajira 35,000 ni za moja kwa moja na zaidi ya 80,000 ni zisizo za moja kwa moja zikijumuisha makundi kama baba na mama lishe, bodaboda, bajaji na watoa huduma za kampuni mbalimbali ya mawasiliano kama vocha, line za simu,” imeeleza taarifa hiyo.

Imeelezwa kuwa utoaji wa ajira hizo ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Serikali kwamba miradi yote ambayo Serikali imewekeza iwe na manufaa kwa Watanzania hususan wale wanaoishi kuzunguka miradi husika na wengine kutokana na ujuzi unaohitajika kwa viwango vya elimu na ujuzi wao.

Mradi wa SGR umetoa fursa za ajira na ujuzi kwa vijana. Mpaka sasa mradi umetoa ajira zaidi ya 35,000 za moja kwa moja kupitia makandarasi na zaidi ya 80,000 zisizo za moja kwa moja katika kipande cha kwanza mpaka cha sita.