Kwa muda mrefu mjadala kuhusu nafasi ya wanawake katika siasa na uongozi nchini umekuwa ukichukua sura mpya kila uchao.
Harakati za kuwatia moyo wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kisiasa zimekuwa zikifanyika kwa hatua zinazolenga kusudio mahsusi.
Leo hii tunashuhudia matunda ya harakati hizo, lakini pia changamoto na wajibu mkubwa uliopo mbele ya wale waliopata nafasi hizo.
Mifano hai ya wale waliothubutu ipo na mingi imekuwa kichocheo kikubwa cha ujasiri miongoni mwa wanawake wanaoendelea kujitokeza kuwania nafasi hizo.
Rais Samia Suluhu Hassan ni mfano hai unaoonyesha jinsi mwanamke anavyoweza kuvunja ukuta wa vikwazo vya kijamii na kisiasa. Alianza kama Makamu wa Rais, nafasi ambayo kwa muda mrefu ilionekana haiwezi kushikiliwa na mwanamke, lakini sasa amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii ni alama kubwa inayowajengea wanawake wengine ujasiri wa kusema, “Kama yeye ameweza, kwa nini mimi nishindwe?”
Lakini itakumbukwa kwa Tanzania, jitihada za kuwahamasisha wanawake kujitokeza kuomba nafasi za uongozi wa kisiasa hazikuanza jana wala juzi.
Ni safari ndefu iliyoasisiwa na watu ikilenga kupanda mbegu ya ujasiri, elimu na kujitambua. Hata kama mbegu hiyo imechukua muda mrefu kuota kama mbuyu au mnazi, leo hii tunaona matunda yake. Hii inatufundisha kuwa mabadiliko ya jambo lolote lile, hayaji mara moja; yanahitaji subira, msukumo wa kudumu na mifano thabiti.
Hata hivyo, ninachokiona katika kutafuta suluhisho kwa jambo hili muhimu ni pale wanawake wanapopata nafasi kubwa za uongozi, jukumu wanalopaswa kulifanya ni kufanya mageuzi ya kisera na kisheria ili kuvunja vikwazo vilivyowachelewesha kwa miongo mingi kuzifikia nafasi hizo.
Hatari iliyopo ni kwamba, wakifika madarakani bila kuleta mabadiliko makubwa, wanaweza kujikuta wamezama kwenye mfumo ule ule uliowafanya wabaki nyuma kwa muda mrefu. Kwa maneno mengine ninayoweza kusema, wanawake hawa lazima wapambanie mifumo itakayosaidia mabadiliko katika kila nyanja badala ya kubaki kama maroboti ndani ya mfumo wa kiume uliowatawala kwa muda mrefu.
Hii inafungua mjadala mkubwa zaidi; je, mafanikio ya mwanamke mmoja ni ushindi wa wote au wa mtu binafsi pekee? Kama wanawake watapata nafasi lakini wasibadili mfumo, basi uwepo wao hautaleta tofauti kubwa kwa Taifa wala kwa wenzao. Kinyume chake, ikiwa watatumia nafasi zao kushughulikia changamoto za muda mrefu za kijinsia, basi itakuwa ni ushindi wa kweli kwao na jamii kwa ujumla.
Hakuna asiyefahamu kwamba historia ya kumkomboa mwanamke kiuongozi, ilianzia Beijing nchini China. Tangu hapo, vyama vya siasa, asasi za kiraia na hata taasisi za kitaifa kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha utoaji wa elimu ya usawa wa kijinsia kwenye uongozi.
Hii ni ishara kwamba mabadiliko ya kijinsia si jukumu la wanawake pekee, bali ni la jamii nzima sambamba na taasisi na Serikali kwa ujumla.
Binafsi nakiri wazi kwamba hatua ya kumteua Samia kwa Makamu wa Rais na hatimaye kuwa Rais wa nchi, imeleta chachu kubwa katika mageuzi ya wanawake na uongozi nchini.
Hata hivyo, nikiri wazi kwamba idadi ya wanawake katika siasa bado hairidhishi. Hili linatupa changamoto ya kuangalia si tu kwenye mifano ya juu kama ya Rais Samia, bali pia kwenye ngazi za chini mfano nafasi ya udiwani, ubunge, uwakilishi na uongozi wa vyama vya siasa. Hapo ndipo pana msingi wa nguvu ya kijinsia. Ukilitazama hili pia kwa jicho la ukuaji wa demokrasia ndani ya vyama, ndipo unaweza kubaini kwamba chanzo cha hamasa kubwa ya wanawake kujitosa kugombea nafasi ambazo zamani hawakuzitamani ndiyo sababu.
Hata hivyo, kazi bado ni kubwa. Vyama vya siasa havina budi kuendelea kutoa nafasi si tu kwa wanawake bali pia kwa makundi mengine kama watu wenye ulemavu na vijana.
Hii ni kwa sababu demokrasia ya kweli haiwezi kutimia ikiwa kundi kubwa la jamii linaachwa nyuma. Kwa mtazamo wangu, hoja zote hizi zinatupeleka kwenye hitimisho moja: mabadiliko ya kijinsia katika uongozi si tukio la ghafla, bali ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji ujasiri wa mifano hai, msukumo wa kijamii na mageuzi ya kisheria na kisera.
Hatua tuliyopo sasa ni ya mpito; tumeshuhudia uwepo wa wanawake katika nafasi kubwa, lakini changamoto kubwa ni kuona kama uwepo huo unaleta mageuzi ya kweli.