Wanaodaiwa kuingiza tani 11 za ‘unga’ waendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, inayowakabili watu saba wakiwemo raia wa Sri Lanka, haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Mosha ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Agosti 20, 2025, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mosha ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Franco Kiswaga, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shitaka linalowakabili halina dhamana.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Riziki Shaweji (40) mfanyabiashara na mkazi wa Masaki,  Andrew Nyembe (34) wakala wa forodha,  Mariam Ngatila (40) mfanyabiashara na mkazi wa Masaki na Ramadhani Said (57) mfanyabiashara na mkazi wa Kifuru.

Wengine ni dereva, Godwin Maffikiri (40) mkazi wa Oysterbay pamoja na wafanyabiashara wawili raia wa Sri Lanka, Jagath Wellalage (46) mkazi wa Kinondoni na Santhush Hewage (25) mkazi wa Masaki.

Katika kesi ya msingi washtakiwa wanadaiwa Julai Mosi, 2025 katika bandari kavu ya Said Salim Bakhresa (SSB- ICD) iliyopo eneo la Sokota Wilaya ya Temeke, kwa pamoja waliingiza sampuli zenye uhusiano na dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, sawa na tani 11.5.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuingiza dawa hizo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Agosti 5, 2025  kesi ya uhujumu uchumi namba 19066 ya mwaka 2025..