Watanzania wajiandae na utekelezaji wa Dira ya maendeleo 2050

Dar es Salaam. Tume ya Taifa Mipango (NPC) inawataka Watanzania kujiandaa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambao utafanyika kwa mtazamo shirikishi na kugusa kila sekta ya maisha ya mwananchi.

Tume hiyo imesisitiza kuwa dira hiyo siyo ya Serikali peke yake, bali ni mwongozo wa pamoja wa kujenga mustakabali wa Taifa unaowahusu watu wa rika zote, mikoa na kada zote.

Dira hiyo itaanza kutekelezwa rasmi katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa na mikakati madhubuti ya kuhakikisha kila Mtanzania anahusika moja kwa moja ama kwa njia ya uzalishaji, matumizi ya rasilimali, elimu, afya, teknolojia, au fursa nyingine zinazolenga kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Utekelezaji wake utakuwa wa kipindi kirefu na kifupi huku kila baada ya mwaka mmoja itafanyika tathmini ya kina kuhusu mafanikio na changamoto zitakazojitokeza.

Akizungumza Agosti 19, 2025 katika Hoteli ya Four Point jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dk Mursal Milanzi amesema utekelezaji huo utafanyika kwa mtindo mpya wa hatua kwa hatua ili kuhakikisha dira hiyo inatekelezeka ipasavyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Tumekuwa hodari kwenye kutunga sera nzuri, lakini utekelezaji wake umekuwa changamoto kubwa. Hii ndiyo sababu tumebadili mkakati kwenye Dira ya 2050. Badala ya kuitekeleza kama kifurushi kimoja kikubwa, sasa tutafanya kwa awamu ya miaka mitano mitano, tukifanya tathmini kila baada ya kipindi hicho,” amesema Dk Milanzi.

Amefafanua kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha kuwa kila hatua inatathminiwa ili kubaini mapema maeneo yenye changamoto na kuyapatia suluhisho kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Jordan Matonya, akitoa maoni yake mbele ya waandishi wa habari katika mkutano huo uliofanyika leo Jumanne Agosti 19, 2025, kwenye Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Dk Milanzi alibainisha kuwa sababu kubwa ya kutokamilika kwa Dira ya Maendeleo 2025 ilikuwa ni athari za janga la Corona (Covid-19), ambalo liliyumbisha uchumi wa dunia na kuathiri utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

“Janga la Corona lilitikisa dunia nzima. Uchumi wa mataifa mengi, ikiwemo Tanzania, ulitetereka kwa kiasi kikubwa. Hili liliathiri utekelezaji wa Dira ya 2025 na hivyo hatukuweza kufikia malengo yote tuliyojiwekea,” amesema.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Jordan Matonya, ameeleza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ni mwongozo muhimu katika kupanga matumizi sahihi ya rasilimali na kuandaa mipango ya maendeleo ya muda mrefu ya Taifa.

“Tunapozungumzia Dira ya 2050 tunamaanisha mwongozo wa pamoja kwa Taifa letu kuelekea miaka 25 ijayo. Kwa mara ya kwanza, utekelezaji wake umejikita katika maoni ya watu zaidi ya milioni 1.1 kutoka sekta mbalimbali. Hii ni ishara njema kwamba dira hii ni ya wananchi wote,” amesema Matonya.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia kwa kiwango kikubwa pamoja na mabadiliko ya fikra za wananchi kuelekea kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo, ni nguzo muhimu kufanikisha malengo ya dira hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi na Kaimu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Melissa Barrett ameeleza kuwa uzinduzi rasmi wa Dira ya 2050 ulifanyika Julai 17, 2025 na Rais, Samia Suluhu Hassan. Alisema dira hiyo inalenga kuleta maendeleo jumuishi, endelevu na thabiti kwa miaka 25 ijayo.

“Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ilionyesha kuwa Tanzania ina watu milioni 61.7. Kwa kiwango cha ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka, ifikapo mwaka 2044 idadi hiyo inatarajiwa kufikia milioni 123. Hii ina maana tunahitaji mipango thabiti kama Dira ya 2050 ili kuhakikisha ukuaji huu wa watu unaendana na maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Melissa.

Ametoa wito kwa Watanzania, hasa vijana, kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hiyo ili Taifa liweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Mipango, malengo ya Dira ya 2050 ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka huo, kila Mtanzania awe na uwezo wa kuzalisha wastani wa Sh18 milioni kwa mwaka. Dk Milanzi amesema lengo hilo linawezekana iwapo kutakuwa na mshikamano na ushirikiano wa dhati kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi.