SIKU chache baada ya Bunda Queens kuachana na wachezaji watatu, inaelezwa wapo kwenye hatua za mwisho kumalizana na Fountain Gate Princess.
Hadi sasa, Bunda imeachana na wachezaji tisa muhimu akiwemo Ester Maseke aliyejiunga na JKT Queens, huku wengine wakiwa ni Mkenya Nelly Kache, Florida Osundwa, Nasra Selemani, Saida Steven, Esther Nyanda, Melkia William, Marry Joseph na Sarah Lucas.
Wachezaji hao ni beki wa kati Sarah Lucas na mabeki wa kushoto Melkia William na Esther Nyanda, wote wakiwa chipukizi waliokulia kwenye akademi hiyo.
Sasa, wakati Bunda yenye makao makuu mkoani Mara ikiagana nao, Fountain Gate inatajwa huenda ikakamilisha usajili wa chipukizi hao kwa ajili ya msimu ujao.
Kiongozi mmoja wa Fountain aliliambia Mwanaspoti kuwa wamevutiwa na wachezaji hao na wanataka kuwaendeleza zaidi ili waje kuwa na manufaa kwa timu na hata Twiga Stars.
“Ukitaja akademi zenye mafanikio kwenye soka la wanawake nafikiri Fountain ni namba moja kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza Simba na Yanga wamepita huku mbali na wale wa nje pia,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Tunaamini wakiwa hapa kama wataonyesha kiwango bora wanaweza kuwa na manufaa makubwa, lakini pia kujiuza nje, kwa sababu Fountain tuna desturi ya kila mwaka kupeleka wachezaji wadogo kujifunza nje.”