BEKI wa zamani wa Simba na Coastal Union, Abdi Banda, ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kusalia Dodoma Jiji baada ya ule wa miezi sita kumalizika msimu huu.
Nyota huyo alijiunga na kikosi hicho Januari 15, 2025 akitokea Baroka FC ya Afrika Kusini, ambako alivunja mkataba miezi mitatu baada ya kuipeleka FIFA timu ya Richards Bay aliyowahi kuichezea kwa madai ya mishahara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Banda, Fadhil Sizya, alisema mchezaji huyo ameamua kubaki Dodoma Jiji baada ya kuwekewa ofa kubwa mara ya pili.
“Nilishauriana na Banda tukakubaliana aongeze mwaka mmoja Dodoma Jiji, sababu walirudi mara ya pili na ofa nzuri kidogo,” alisema na kuongeza:
“Amazulu ya Afrika Kusini walikuwa wanamtaka. Kocha wao msaidizi Simon Dladla nilishakubaliana naye, walitaka wamuone kwenye mazoezi, lakini baada ya ofa nzuri akaamua kubaki Bongo.”
“Japo Banda angeweza kufanya majaribio na kufuzu, lakini Dodoma aliishi nao vizuri sana. Waliporudi mara ya pili ilikuwa ngumu kuwakatalia kwa sababu wamekuwa wakarimu na wanampa heshima kubwa sana.”
Beki huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali amecheza kwa misimu tofauti Baroka, Chippa United, Highlands Park na TS Galaxy nchini Afrika Kusini.