ACT-Wazalendo yamjibu msajili hoja za Monalisa

Dar es Salaam. Sakata la uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo limeendelea kushika kasi,  huku  chama hicho kikitoa majibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Naibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala anayepinga uteuzi huo.

Monalisa aliwasilisha malalamiko hayo Agosti 19, 2025 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huku nakala akiiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), pamoja na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu.

Chanzo cha malalamiko ya kada huyo, anadai ni hatua ya chama chake kumteua Mpina kuwa mgombea wa urais siku moja tu baada ya kujiunga rasmi na ACT-Wazalendo (Agosti 5, 2025) na Agosti 6, 2025 akapitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa kuwa mgombea wa kiti hicho.

Monalisa anadai hatua hiyo inakiuka kanuni za kudumu za uendeshaji wa chama, akikitaja Kifungu cha 16(4)(I,III na IV) cha toleo la mwaka 2015, zinazotaka mgombea wa nafasi ya juu kitaifa awe mwanachama kwa angalau mwezi mmoja kabla ya mwisho wa mchakato wa uteuzi.

Hata hivyo, awali akizungumza na Mwananchi kuhusu sakata hilo, Ado alisema masuala hayo ni ya ndani ya chama na aghalabu hushughulikiwa kupitia vikao vya ndani, akieleza kushangazwa na hatua ya suala hilo kuwasilishwa kwa msajili.

Hata hivyo, Leo Agosti 21, 2025 Mwananchi ilipomuuliza, Ado kuhusu kuwasilisha barua ya majibu kwa Msajili, amekiri kufanya hivyo, ingawa hakufafanua zaidi.

Kutokana na malalamiko hayo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa juzi ilitoa saa 30 kwa ACT-Wazalendo kujibu rasmi malalamiko ya Monalisa.

Akizungumza leo Agosti 21, 2025 baada ya kutafutwa na Mwananchi kujua nini kinachoendelea, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza amethibitisha kupokea barua ya majibu ya Chama cha ACT-Wazalendo tangu jana, huku akisema tayari ofisi yake imemtaka Monalisa kutoa maelezo ya ziada kabla ya uamuzi rasmi kutolewa.

“Tumemwandikia Monalisa barua nyingine ili atoe maelezo ya ziada na kesho ndiyo siku ya mwisho kuwasilisha maelezo hayo. Baada ya hapo, tutawaita pande zote mbili kwa mazungumzo kabla ya kutoa msimamo wetu,” amesema Nyahoza.

Monalisa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu barua hiyo ya Msajili, amekiri kuipokea na kueleza kuwa anaitafakari.

Amesema iwapo hataridhika na majibu yaliyotolewa na chama chake, atawasilisha maelezo ya ziada kama alivyoelekezwa.

“Nipo njiani naelekea kwa msajili kuchukua hiyo barua. Nitaisoma ili kujua majibu yaliyotolewa na chama na kama nitayaona yana upungufu, basi nitatoa maelezo ya ziada kama nilivyoelekezwa,” amesema Monalisa.