Ahofiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi mgodini

Bunda. Mtu mmoja anahofiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi katika shimo linalotumika kuchimba dhahabu katika mgodi wa Kinyambwiga, eneo la Walwa lililopo Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Mtu huyo aliyetambulika kwa jina la Juma Lutalamura, mkazi wa Katoro mkoani Geita ambaye ni fundi, amekumbwa na tukio hilo akiwa anafanya matengenezo ya shimo hilo.

Tukio hilo limetokea Agosti 19, 2025 saa 10 jioni wakati fundi huyo alipokuwa akifanya matengenezo ya shimo moja kabla ya kufunikwa na kifusi.

Matengenezo hayo yalihusisha ubadilishaji wa mbao zilizopo kwenye shimo hilo kwa kutoa mbao za zamani na kuweka mbao mpya.

“Alikuwa anafanya matengenezo ya kawaida kwani huwa tuna utaratibu wa kufanya matengenezo pale tunapoona miti au mbao za kwenye duara zimeoza, bahati mbaya kifusi kikamfunika,” amesema Palapala Mashauri ambaye ni mmiliki wa shimo hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 21, 2025, Mashauri amefafanua kuwa baada ya fundi huyo kufukiwa, awali alikuwa akiwasiliana na watu walio nje akiwalekeza sehemu alipo ili aweze kuokolewa lakini uokoaji ukawa ni mgumu kwani kila walipokuwa wakichimba mchanga ulikuwa unaonyesha dalili za kuporomoka.

Amesema ugumu huo ulitokana na eneo hilo kutitia kila wanapojaribu kuchimba hali iliyokuwa ikitishia usalama wa waokoji, ndipo wakaamua kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya usaidizi zaidi.

“Alikuwa anelekeza alipo lakini kila tukijaribu kuchimba kifusi kilikuwa kinaonyesha dalili za kuporomoka kwani eneo lilikuwa linatitia, tumehangaika usiku kucha bila mafanikio na sasa hatuna mawasiliano naye, sina uhakika kama bado yuko hai,” amesema Mashauri.

Uokoaji ukiendelea katika mgodi wa Kinyambwiga eneo la Walwa wilayani Bunda baada ya fundi kufukiwa na kifusi akiwa anafanya matengenezo ya shimo la kuchimba dhahabu



“Mimi nilibaki kwa juu kidogo, yeye (Juma) alishuka chini kabisa, ghafla kamba ikakatika na mbao zikamfunika pamoja na mchanga, mimi kilichoninusuru nilikuwa kwenye bomba huku juu nikahangaika hadi nikatoka nje huku yeye akishindwa kwa sababu ule mdomo wa duara ulikuwa umefunikwa kabisa,” amesema Iddi Mweli.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Agostino Magere amesema jitihada za kumuokoa mtu huyo bado zinaendelea huku akiwataka wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa kuzingitia masuala ya usalama mahali pa kazi.

“Utafutaji mzuri ni ule ambao unamaliza ukiwa salama, unapata pesa yako na kuitumia ukiwa salama. Wachimbaji wanatakiwa kuepuka mazingira ya aina yoyote yanayoashiria hatari, Serikali inapenda kuwaona watu wake wakifanya shughuli zao huku wakiendelea kuwa salama muda wote,” amesema Magere.

Amesema tayari jeshi hilo limefika eneo la tukio ambapo shughuli ya uokoaji inafanyika kwa ushirikiano kati ya askari wa Zimamoto na wachimbaji.