BARRICK NORTH MARA YAPELEKA KICHEKO,TABASAMU LA MAJI VIJIJI 11 WILAYANI TARIME

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi akijaribu maji yanayotiririka kwenye bomba jipya la mradi wa chanzo cha maji na kupeleka maji Kijiji cha Kewanja , Nyamongo, Wilaya ya Tarime vijijini.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi (kushoto) akizindua jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa zahanati ya Mangucha ambayo inajengwa kwa fedha za CSR zilizotolewa na mgodi.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ismail Ali Ussi (Kulia) akiwa ameshika mwenge wa uhuru pamoja na Meneja wa Mgodi wa Barrick North Mara Apolinary Lyambiko kwenye uzinduzi wa upanuzi wa mradi wa chanzo cha maji na kupeleka maji Kijiji cha Kewanja , Nyamongo, Wilaya ya Tarime vijijini.

#Yafanikisha mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 2.6

MAJI ni bidhaa adimu kwa miaka mingi katika maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini. Tatizo hilo linaathiri maisha ya wananchi na uchumi wa nchi.

Hata hivyo, serikali inajitahidi sana kutatua tatizo hilo katika maeneo mbalimbali, kwa kushirikiana na wahisani na wadau mbalimbali mfano kampuni ya Barrick inayoendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga.

Mgodi wa Barrick North Mara kupitia fedha za CSR umefanikisha mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 2.665 kwa ajili ya upanuzi wa chanzo cha maji cha Nyamongo, wilayani Tarime vijijini kilichopo ndani ya eneo la Mgodi ambacho awali kilisanifiwa kuhudumia wananchi 27,742 wa vijiji vya Nyangoto, Matongo, Mjini Kati na Nyabichune.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika vijiji vingine saba vinavyozunguka mgodi. Chanzo hiki kimesanifiwa upya kwa lengo la kuhudumia wananchi 125,566 katika vijiji vingine sita vya Genkuru, Nyamwaga, nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera.Mgodi pia unaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi za Zahanati katika kijiji cha Mangucha.

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameupongeza mgodi wa Barrick North Mara, kwa kufanikisha mradi huu mkubwa wa maji na kuendelea kuwa kielelezo cha mwekezaji bora kwa kutekeleza kwa vitendo miradi ya maendeleo kupitia kanuni ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ismail Ali Ussi akizungumza na wafanyakazi wa Barrick North Mara na wananchi

“Kampuni ya Barrick ni moja ya wawekezaji wenye nia na dhati kwa maslahi mapana ya nchini yetu , Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, alifungua milango kwa ajili ya wawekezaji wa nje aina ya Barrick kwa sababu ni wawekezaji wazuri kwa ustawi wa taifa letu na watu wake, ”amesema Ussi.

Ameongeza kuwa eneo la Mgodi wa Barrick North Mara, ni sehemu ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na wakazi wa Nyamongo, vijiji na vitongoji vyake kupitia mradi huu wakazi hawa watapata maji safi na salama na kuondoa adha na tatizo la maji la muda mrefu,

Ussi amechukua nafasi hiyo kwa kuwapongeza pia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Wizara ya Maji kwa kufanya kazi kwa bidii , uzalendo na uadilifu katika kuwatumikia watanzania kwa niaba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake , Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) , Mhandisi Mohammed Mtopa Athumani, amesema mradi huu wa upanuzi wa chanzo cha maji una lengo la kusambaza maji katika vijiji saba na kupeleka maji Kijiji cha Kewanja.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi akijaribu maji yanayotiririka kwenye bomba jipya la mradi wa chanzo cha maji na kupeleka maji Kijiji cha Kewanja , Nyamongo, Wilaya ya Tarime vijijini.

Athuman amesema mradi huo utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 2,314,000 millioni hadi lita 10,213,000 millioni na kufikia lengo la serikali la mwaka 2020-2025 la 85% ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio vijijini.

Amefafanua kwamba mradi huo ulianza 21/02/2025 na unatarajiwa kukamilika 18/10/2025 na umefikia 80% katika utekelezaji wake katika kuhakikisha adha ya matatizo ya maji yanapungua na kumalizwa kabisa katika sehemu za vijijini.

“Kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa kitako cha tanki ya kukusanyia maji, usimikaji wa tanki zenye ujazo wa lita laki mbili, ulazaji wa bomba la kutoka kwenye chanzo mpaka kwenye tanki za kukusanyia maji, ununuzi na ufungaji wa pampu, ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba kuu la kupandisha maji km1.5”, amesema Mhandisi Athuman.

Wananchi wa maeneo mbalimbali yatakayonufaika na mradi huo wamepongeza kufanikishwa kwa mradi huo mkubwa utakaomaliza kero ya ukosefu mwa maji.

Sehemu ya wakazi wa Mangucha na vitongoji vyake

Zainab Maulid, ni mama wa watoto watatu, mkazi wa Kijiji cha Nyamongo. Yeye anasema kwa miaka mingi tangu akiwa msichana, alizoea kuamka alfajiri kufuata maji mbali na hiyo ilikuwa ndiyo ratiba yake ya kila siku. Anasema shida hiyo ilimwathiri yeye na wanakijiji wenzake kwa miaka mingi.

Lakini, anasema hivi sasa yeye ni mwenye kicheko na furaha ya ajabu, kutokana na shida hiyo ya maji kutatuliwa. Anaeleza kuwa Barrick North imewezesha waanze kupata maji safi na salama katika awamu ya kwanza ya mradi huu na kufanya kero ya maji kuwa historia.

“Tulikuwa tunateseka kwa shida ya maji, lakini sasa tutaokoa muda kwa kufanya shughuli zingine za kiuchumi. Tunaishukuru Barrick North Mara kwa kuleta majisafi kwenye makazi yetu hapa Nyamongo na kwenye vijini vingine vinavyozunguka Mgodi”, amesema Zainab huku akitabasamu.

Meneja wa Mgodi wa Barrick North Mara ,Apolinary Lyambiko, anafafanua kuwa mradi huu ni moja ya miradi mingi inayotekelezwa na fedha za CSR zinazitolewa na Mgodi katika maeneo ya vijiji vinavyouzunguka inayonufaisha wananchi.

Barrick ni kampuni kubwa iliyowekeza katika uchimbaji wa madini ya dhahabu nchini kupitia migodi yake ya North Mara,Bulyanhulu na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa na ina progamu madhubuti za kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha sekta mbalimbali hususan elimu, afya,kuboresha miundombinu na mazingira kwa lengo la kuinua maisha ya wananchi.

Sehemu ya wafanyakazi wa Barrick North Mara