Biteko aagiza minada yote kutumia nishati safi

Dodoma. Ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mkakati wake, Serikali imeagiza minada yote nchini kutumia nishari safi ya kupikia, ikianza na majiko ya kisasa ya kuchomea nyama kwenye mnada wa Msalato mkoani Dodoma, yanayotumia mkaa mbadala.

Akizungumza leo Agosti 21, 2025 kwenye hafla ya uhamasishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wadau wanaochoma nyama mnadani hapo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema mnada wa Msalato utakuwa mfano wa mingine nchini katika matumizi ya nishati hiyo.

Dk Biteko amesema lengo la kupeleka majiko hayo minadani siyo kubadilisha mazingira ya minada, bali kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa makundi mbalimbali.

‎Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameibeba ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika, hivyo Tanzania ni lazima iwe kinara wa matumizi hayo.

‎‎”Nchi mbalimbali zinakuja Tanzania kujifunza matumizi ya nishati safi ya kupikia, sasa wanapokuja minadani na kukutana na matumizi ya mkaa na kuni wanaona hatuko serious (makini) na suala hili, ndiyo maana tumechukua hatua,” amesema.

 ‎‎‎”Kuna mtu mmoja aliwahi kuniambia kuwa, raha ya kula nyama mnadani ni vumbi linakuja halafu unajipangusa, umekaa unakula nyama kuna paka anakatisha unataka kukimbia, hayo ndiyo mazingira ya minada. Hatutaki kuyabadilisha yawe kama hoteli, mazingira yatabaki vilevile ila tunataka watumie nishati safi ya kupikia wanaochoma nyama na kupika vyakula.”

‎Ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (Stamico) linalotengeneza mkaa mbadala unaotumika kwenye majiko sanifu na kuchomea nyama, kuhakikisha unapatikana muda wote ili watumiaji wasipate visingizio vya kutumia mkaa na kuni. Pia, ameagiza mama lishe wapewe uwakala wa mkaa huo ili upatikane muda wote.

‎Mbali ya hayo, ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuhakikisha majiko ya kuchomea nyama kwa kutumia nishati safi ya kupikia yanapatikana haraka ili yaanze kutumika.

‎Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2022 hadi asilimia 20.3 mwaka 2025.

‎‎Serikali inatekeleza mkakati wa miaka 10 ulioanza mwaka 2024 unaolenga ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wameondokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.

Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Hassan Said amesema kuwashawishi wachoma nyama na mama lishe kutumia nishati safi ya kupikia halikuwa jambo rahisi kwa kuwa, asilimia 90 walikuwa hawaelewi kuhusu nishati hiyo na asilimia 20 walikuwa hawajawahi kabisa kusikia kuhusu nishati safi.

‎‎Amesema walitoa elimu ya matumizi hayo na mwisho wa siku walikubaliana kubadilika.

‎Mwenyekiti wa wachoma nyama katika mnada wa Msalato, Mathias Raphael ameiomba wizara kuwahakikishia upatikanaji wa mkaa mbadala kwa kuwa, hawajui mahali pa kuupata.

‎‎Amesema majaribio ya majiko yameonesha inawezekana kutumia mkaa mbadala ambao ni gharama ndogo, lakini nyama inaiva vizuri bila moshi, majivu wala uchafu wowote na ladha yake ni nzuri.

‎Wakati huohuo, Kampuni ya ORYX Energies Tanzania kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa nishati imezindua mfumo wa usambazaji gesi ya LPG katika Soko la Samaki Feri, jijini Dar es Salaam.

Mfumo huo unatumia teknolojia ya malipo ya kulipia kadri ya matumizi (kama ilivyo Luku kwa umeme), jambo linalowaondolea mzigo wa kununua mitungi ya gesi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kampuni hiyo imeweka matangi ya gesi ardhini na mtandao wa mabomba unaohudumia majiko 48 yaliyopo sokoni hapo, kila moja likiwa na mita yake ya kusoma matumizi ya kila siku.

Mkurugenzi Mkuu wa ORYX Energies Tanzania, Araman Benoit amesema mradi umegharimu Sh250 milioni.