:::::::;
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN Women), Bi. Anna Mutavati, anayefanya ziara ya kikazi nchini tarehe kuanzia 18–20 Agosti 2025.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam na yalilenga kujadili nafasi ya Tanzania katika kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia ili kuwainua Wanawake kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa Mpango wa Generation Equality, Beijing +30 Action Agenda, pamoja na vipaumbele vya Tanzania katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Chumi ameeleza nia na mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuimarisha usawa wa kijinsia nchini. Mhe. Chumi ameeleza kuwa kupitia katiba na sera mbalimbali, ikiwemo Sera ya Taifa ya Usawa wa Kijinsia na Maendeleo ya Wanawake (2023), maboresho ya sheria dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kitaifa serikali itaendelea kutimiza jukumu lake la kuhakikisha inawainua wanawake kimaendeleo.
Aidha, amebainisha kuwa Tanzania ni mwanachama wa mikataba na ahadi za kikanda na kimataifa ikiwemo CEDAW, Itifaki ya AU kuhusu Haki za Wanawake, Itifaki ya SADC ya Usawa wa Kijinsia, Ajenda ya 2063 na SDGs za 2030.
“Kama Taifa, tumeendelea kusimama mstari wa mbele katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa, na tunaamini ushirikiano wetu na UN Women utaongeza nguvu katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye uongozi, uchumi, amani na ulinzi, sambamba na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,” alisema Mhe. Chumi.
Kwa upande wake, Bi. Mutavati amepongeza uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuendeleza ajenda ya Generation Equality na kubadilisha maisha ya wanawake kupitia fursa za kiuchumi, ushiriki wa kisiasa na ulinzi wa kijamii.
Ameeleza kuwa UN Women inaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia miradi mbalimbali kama vile Wanawake Wanaweza, Women’s Leadership and Economic Rights (WLER), uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali kupitia Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), mpango wa African Girls Can Code (Binti Dijitali), na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Azimio 1325 kuhusu Wanawake, Amani na Usalama (TNAP-WPS).
Amebainisha kuwa UN Women itaimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika maeneo ya bajeti jumuishi yenye mtazamo wa kijinsia (Gender Responsive Budgeting), uimarishaji wa takwimu za kijinsia kwa ajili ya sera shirikishi, na kuendeleza juhudi za kumaliza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kupitia miradi inayotekelezwa Zanzibar, Pemba na Tanzania Bara.
Kupitia mazungumzo hayo, pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha uongozi wa kikanda na kimataifa wa Tanzania katika ajenda ya usawa wa kijinsia, kuongeza uwekezaji katika uwezeshaji kiuchumi wa wanawake, na kuhakikisha makundi yenye uhitaji maalum kama wanawake wa vijijini, wenye ulemavu, wenye ualbino, wafugaji na wanawake wanaoishi na VVU hawanachwa nyuma.
Pia wamekubaliana kuunga mkono uzinduzi na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Wanawake, Amani na Usalama (TNAP-WPS) utakaofanyika Agosti 2025, kama ishara ya uongozi wa Tanzania katika ajenda ya kimataifa ya amani endelevu na usawa wa kijinsia.
Bi. Mutavati aliambatana na timu ya wataalamu wa UN Women Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini.