Itilima. Hofu imetanda kwa wakazi wa Kijiji cha Gambasingu baada ya fisi wanne kuvamia zizi la kondoo na kuua kondoo 17 huku wengine watano wakijeruhiwa katika shambulio la usiku wa kuamkia leo Agosti 21, 2025.
Shambulio hilo lilitokea saa 6 usiku katika Kitongoji cha Mwabasambo A na limeelezwa na wenyeji kuwa ni tukio la kihistoria kutokana na idadi kubwa ya mifugo kushambuliwa kwa wakati mmoja.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 21, 2025 kijijini hapo, Singisi Mgina, mfugaji aliyeathiriwa na fisi hao, amesema fisi hao walivamia zizi lake kwa kasi na kuua kondoo kabla hajapata msaada.
“Walivamia ghafla na kuua kondoo kwa muda mfupi. Nilipopiga kelele, wananchi walifika lakini tulishindwa kuwafukuza. Hasara yangu ni kubwa, inafikia Sh2 milioni. Kondoo hawa ndio chanzo cha kipato cha familia yangu,” amesema.
Amesema wakati fisi hao walipokuwa ndani ya zizi hilo, alisikia namna walivyokuwa wakipambana kujiokoa lakini walizidiwa na fisi hao ambao baadaye alibaini walikuwa wanne.
Mussa Masalu, mkazi wa kijiji hicho, amesema hajawahi kushuhudia fisi kushambulia kwa idadi kubwa ya mifugo kwa wakati mmoja.
“Hii ni hatari kubwa. Kama wanaweza kuua kondoo wengi kwa muda mfupi, kesho wanaweza kushambulia hata watu. Tunaiomba Serikali iingilie kati mara moja,” amesema.
Naye Ngolo Machibya ameongeza kuwa mifugo ndiyo uti wa mgongo wa familia nyingi, hasa wanawake.
“Kondoo ni mali ya familia na kipato chetu cha kila siku. Tukio hili linatupa hofu kubwa, hasa kwa watoto wanaotembea usiku. Tunaishi kwa wasiwasi mkubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Gambasingu, Buka Maduhu amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa idadi kubwa ya kondoo waliouawa inaashiria ukali wa tatizo.
“Matukio ya fisi kushambulia mifugo yamewahi kutokea miaka ya nyuma, lakini hili ni kubwa kuliko yote. Inaonyesha wanyama hawa wana njaa. Mazizi yenye mbwa hulindwa zaidi kwa kuwa fisi huwa na hofu,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Itilima, Nelson Kira amesema Serikali imeanza msako kwa kushirikiana na wananchi na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
“Tumeshaanza kuchukua hatua kudhibiti fisi hao kabla hawajasababisha madhara zaidi. Wananchi wanashauriwa pia kuimarisha ulinzi wa mazizi yao,” amesema.
Katika wilaya ya Itilima kumekuwa na matukio mengi ya fisi kuvamia makazi ya watu na hivi karibuni watoto tisa waliuawa na fisi na msako ulianzishwa kuwasaka fisi hao na fisi 15 kuuawa huku mmoja akibainika kuwa na namba kwenye paja iliyoandikwa “INALA 7”.