Dar es Salaam. Foleni ya magari katika maeneo ya Kamata na Buguruni, imemkera Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kiasi cha kumfanya atoe maagizo kwa watendaji wa wizara.
Ulega amesema hayo leo, Alhamisi Agosti 21, 2025 jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kumtunuku tuzo maalumu Rais Samia Suluhu Hassan, iliyotolewa na makandarasi nchini kwa kuthamini mchango wake kwenye sekta ya ujenzi tangu aingie madarakani miaka minne iliyopita.
Waziri huyo amemwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Musonde, na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta, kukaa na wataalamu na kutoa mapendekezo kwake kuhusu hatua za kuchukua ili kupunguza foleni katika maeneo hayo.

Amesema maeneo hayo mawili yamekuwa chanzo kikubwa cha foleni katikati ya jiji, huku akisema kukamilika kwa ripoti hiyo kutaifanya Serikali ichukue hatua za haraka ili kuondokana na hali hiyo.
Akizungumzia tuzo hiyo ya Rais Samia aliyoipokea kwa niaba yake, Waziri Ulega amesema uamuzi wa makandarasi kumpatia tuzo Rais ni kwa sababu mambo aliyoyafanya katika sekta ya ujenzi ni makubwa na yanaonekana wazi.
Akizungumza kwa kutoa mifano, Ulega amesema ujenzi mkubwa wa barabara na madaraja umefanyika ndani ya miaka minne iliyopita na kuweka rekodi ya aina yake.
“Wakati mwingine sisi ambao tunaishi Tanzania hatuoni au tunaweza kubeza kile kilichofanyika. Lakini juzi hapa, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, amesema siku hizi anapotea akija Dar es Salaam kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya kimiundombinu yanayoendelea,” amesema waziri huyo.
Kuhusu uwezeshaji wa makandarasi wazawa, Waziri Ulega amesema tayari Serikali inatekeleza hilo na kuna miradi ambayo wanaitekeleza kwa upendeleo yenye thamani isiyozidi Sh50 bilioni.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega (katikati), akipokea tuzo ambayo wakandarasi nchini wamemzawadia Rais Samia Suluhu Hassan kutokana maendeleo makubwa aliyoyafanya katika sekta ya ujenzi nchini. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chemba ya Wakandarasi na Miundombinu nchini (CCIT), Pamela Shoo na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa CCIT, Stephen Mkomwa. Mpigapicha Wetu
Amesema kitendo hicho kimeonesha pia kwamba Serikali inatamani kuona wazawa wakipata kazi zaidi.
Kuhusu mchango wa sekta ya ujenzi nchini, amesema ni moja ya misingi muhimu ya maendeleo ya nchi, ikichangia asilimia 16 ya Pato la Taifa, huku takribani ajira milioni 1.8 zikizalishwa kupitia sekta hiyo.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Wakandarasi na Miundombinu (CCIZ), Steven Mkomwa, amesema sekta hiyo imepata maendeleo makubwa katika miaka ya karibuni, ingawa kuna changamoto zinahitaji kufanyiwa kazi.